Header Ads

Balozi Amina: Bado nautaka urais.



Balozi Amina Salum Ali .
Balozi Amina Salum Ali . 
Amina Salum Ali, ambaye alishika nafasi ya pili kwenye mbio za urais ndani ya CCM, amesema ndoto yake ya kushika nafasi hiyo ya juu katika siasa nchini, haijafa.
Amina, ambaye alikuwa balozi wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, alisema hayo kwenye mahojiano maalum na Mwananchi yaliyofanyika mapema wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Balozi Amina alichomoza kwenye mbio za urais ndani ya CCM baada ya kuingia tano bora, akiwa pamoja na John Magufuli, Asha Rose Migiro, January Makamba na Bernard Membe na baadaye kuingia tatu bora kwa ajili ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa chama hicho ambao ulimchagua Magufuli kugombea urais.
Lakini Balozi Amina, ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 59, anasema hilo halijaondoa ndoto yake ya kuingia Ikulu.
“Sikushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka jana kwa ajili ya kujaribu bahati yangu, bali nilikuwa na nia ya dhati ya kushinda urais na kuwatumikia wananchi,” alisema Balozi Amina.
“Sikushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka jana kwa ajili ya kujaribu bahati yangu, bali nilikuwa na nia ya dhati ya kushinda urais na kuwatumikia wananchi,” alisema Balozi Amina.
“Nilitamani kweli niwe rais na niseme tu kwamba kwa kweli ndoto yangu hiyo haijafa, ingawa jambo hilo sasa litategemea muda, uhai, afya na mazingira yatakayojitokeza baada ya Rais Magufuli kumaliza muhula wake wa uongozi,” alisema.
Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM, kada anayechaguliwa kuwa Rais hupitishwa tena kugombea urais baada ya kipindi chake cha miaka mitano kumalizika ili aongoze nchi kwa vipindi viwili.
Balozi Amina anasema safari yake ya kuelekea Ikulu ilikumbwa na vikwazo viwili, ambavyo alivitaja kuwa ni Watanzania kutokuwa tayari kuongozwa na mwanamke na pia mchakato wa uchaguzi kutawaliwa na wenye fedha.
Alisema bado jamii haijawa tayari kuamini kuwa mwanamke anaweza kuwa kiongozi wa juu wa ngazi kama ya urais, lakini anasema jitihada za CCM kwenye uchaguzi uliopita kumkubali mwanamke zinaweza kubadilisha mtazamo wa jamii.
“Mimi naona tatizo hilo limesababishwa na mambo mengi. Inaweza ikawa tatizo la elimu kwamba watu bado hawajaelewa vya kutosha kwamba mwanamke anaweza,” alisema.
“Lakini pia hili ni suala la mila na desturi. Kuna baadhi ya maeneo nchini mwanamke hachukuliwi kama ana mchango wowote katika maendeleo ya jamii. Lakini ninavyoona hali hii itakwisha na tumeanza kuimaliza baada ya kumpata Makamu wa Rais Mwanamke.”
Amina alibainisha kuwa mawazo kwamba mwanamke hawezi kuwa kiongozi ni potofu, ingawa na yametokana pia na ukweli kwamba baadhi ya wanawake hawajajitambua vya kutosha.
“Kuna uwezekano Tanzania ikaongozwa na mwanamke na watu waondoe mawazo kuwa mwanamke hafai kuwa kiongozi. Wanawake wana uwezo mzuri, ila wanachohitaji kutoka kwa jamii ni kuwaamini tu,” alisema.
Jambo jingine ni mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia CCM, na hasa nafasi ya Urais.
Alisema utaratibu unaotumika sasa kuanzia uchukuaji wa fomu mpaka uteuzi, unatengeneza makundi ya walionacho na wasionacho ndani ya chama hicho na hivyo kuwafanya baadhi ya wanachama kushindwa kukabiliana na ushindani.
“Chama kiimarishe process (mchakato) za kutafuta wadhamini, kiangalie upya mfumo na ikiwezekana turudi kwenye mfumo wa zamani wa kamati ya utendaji kuwachuja wagombea,” alisema Kuhusu mkakati wake endapo angepitishwa na baadaye kuchaguliwa kuwa Rais, Balozi Amina alisema alitaka wananchi wanufaike na kukua kwa uchumi.
“Nilitaka nitafsiri kukua kwa uchumi mifukoni mwa wananchi,” alisema.
Amina alisema haina maana kueleza kuwa uchumi wa nchi unakua wakati Watanzania bado wanaishi maisha ya umaskini na hicho ndicho kilikuwa kilio chake.
Alieleza wakati sera zikielekeza kuhusu viwanda na kilimo, dira yake ingekuwa kusimamia uboreshaji wa mazao ya kilimo na viwandani ili yaongezwe ubora kabla ya kuuzwa, kitu ambacho alisema kingesaidia kuongeza ajira kwa vijana.
“Nilitamani kuona kama tunazalisha mazao ya kilimo, tuyasindike kwanza kabla ya kuuza. Na bidhaa za viwandani hivyo hivyo ili tuongeze ubora na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaongeza ajira kwa vijana,” alisema.
Pia, alisema angesimamia ukusanyaji wa kodi kama inavyofanywa sasa na Serikali ya Rais Magufuli, lakini yeye asingeishia kusimamia makusanyo ya kodi inayoingia kupitia bandari pekee, bali angetafuta vyanzo mbadala vya uhakika vya kuongeza mapato ya Serikali.
“Kukusanya mapato bandarini ni sawa, lakini bandari si chanzo cha mapato cha kutegemea sana, kwani bidhaa zinaingia bandarini kama dunia haijachafuka. Ikitokea machafuko kwenye nchi ambazo zinatumia bandari zetu hatuwezi kupata mizigo ya kuitoza kodi. Kumbe ningetafuta vyanzo vingine vya uhakika zaidi vya mapato,” alisema.
Uchaguzi Mkuu ulikuwa huru na wa haki
Kuhusu tathmini ya uchaguzi, Balozi Amina alisema ulikuwa huru kwa vigezo vyote vya ndani na nje ya nchi.
“Uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na hata Umoja wa Mataifa unatambua hilo. Pia waangalizi mbalimbali wa kimataifa walieleza kuwa uchaguzi ule haukuwa na shida,” alisema.
CHANZO:MWANANCHI

No comments