Askofu Mpya KKKT Aonya Utumbuaji MAJIPU.......Amtahadharisha Rais Kutumbua Majipu kwa Haki, Asema Bunge Halipaswi Kulindwa na Jeshi
(Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo (kulia) na Askofu Mkuu wa KKKT Mstaafu Alex Malasusa baada ya ibada ya kumuingiza kazini Askofu Shoo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la KKKT mjini Moshi Januari 31, 2016. )
***
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo ameitahadharisha Serikali kuhusu zoezi la Utumbuaji Majipu linaloendelea akiitaka kuzingatia misingi ya haki na busara ya Ki-mungu ili kutowapa nafasi watu wasio waaminifu kuitumia vibaya kufanya ukandamizaji.
Askofu Shoo aliyasema hayo jana mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro, katika ibada maalum ya kuingizwa kazini iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema kuwa Kanisa lina imani na Serikali ya Awamu ya Tano na kupongeza juhudi zake katika kupambana na watumishi wa wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali za umma pamoja na mafisadi, lakini zoezi la kutumbua majipu linapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka uonevu.
“Utumbuaji huu ufanyike katika misingi ya haki na kwa busara kwani watu wengine wanaweza kutumia mwanya huu kuonea wenzao wasiokuwa na hatia,” alisema Askofu Shoo.
Katika hatua nyingine, Askofu Shayo alielezwa kusikitishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya wabunge wanapokuwa Bungeni.
“Tunahitaji kuona Bunge linajadili vikao vyake kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia. Kanisa linasikitishwa sana na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyoendelea bungeni. Tunapenda kuona hoja zinajadiliwa kwa ustaarabu,” alieleza.
Kadhalika, Askofu Shayo aliionya matumizi ya jeshi la Polisi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza kuwa Bunge ni sehemu ya Demokrasia na kamwe haipaswi kulindwa na jeshi. Aliongeza kuwa Bunge linapaswa kuendeshwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na uwazi.
Aliihakikishia serikali kuwa Kanisa litaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo ikiwa ni pamoja ikiwemo sekta ya elimu na afya. Aliishauri Serikali kuangalia upya sera ya elimu bure na kuboresha utoaji wa elimu hiyo.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizishukuru taasisi za dini kwa kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo kupitia sekta mbalimbali na kuzihimiza kuendelea kuwekeza katika maeneo muhimu yakiwemo ya Afya na elimu.
“Napenda kutumia fursa hii kuyashukuru madhehebu ya dini ambayo yamekuwa mstari wa mbele kusaidia Serikali katika kufikisha huduma hizi za afya karibu zaidi na wananch. Wito wangu kwa hili, naombeni mjitahidi kutoa huduma hizi kwa gharama nafuu ili wananchi wengi waweze kuzitumia,” Waziri Mkuu Majaliwa ananukuliwa.
Ibada hiyo maalum ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Post a Comment