Wakuu wa Mikoa na Wilaya Kupukutishwa.
Baada ya kutaja Baraza la Mawaziri lenye sura mpya nyingi juzi ikiwa moja ya hatua katika ukamilishaji wa safu za uongozi wa serikali ya awamu ya tano, Rais John Magufuli anataraji kuondoa Wakuu wengi wa Mikoa na Wilaya kutokana na kukosa sifa, taarifa za uhakika zinasema.
Mbali na wawakilishi wa Rais hao katika ngazi ya Mkoa na Wilaya, panga kubwa litawakumba wakurugenzi wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini.
Taarifa kutoka ndani ya serikali zinaeleza kuwa Rais Magufuli ameshaitisha mafaili ya kumbukumbu za wasifu wa viongozi hao ili kujiridhisha na sifa zao.
Chanzo cha habari kutoka serikalini kimedokeza kuwa taasisi na mashirika ambayo yapo katika hatari ya kukumbwa na fagio la Rais Magufuli ni pamoja na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Taarifa zilieleza kuwa Rais Magufuli atachukua hatua hiyo kwa lengo la kuteua watendaji wapya ambao wataendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano inayotekeleza kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.
“Unajua ma RC na ma DC wakati wa serikali ya awamu ya nne baadhi walipewa nafasi hizo kwa huruma ya kukosa ubunge ndiyo sababu baadhi yao wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” kilisema chanzo hicho.
Fagio hilo litawahusisha pia watendaji ambao wakati wa serikali ya awamu ya nne walivurunda katika sehemu zao za kazi na kilichofanyika ni kuwahamisha na kupangiwa maeneo mengi.
Wakati wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ulikuwa ukipokelewa kwa hisia tofauti na wasomi na wanasiasa.
Wengi walidai hiyo imekuwa kama kichaka cha kuwahifadhi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho .
Post a Comment