Vigogo 15 mbaroni Bukoba.
WATUMISHI 15 wa Idara za Ardhi, Mipango Miji na Ujenzi katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera akiwemo Msanifu wa Majengo wa Manispaa hiyo, Abukar Issa, wanashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi dhidi ya tuhuma za kugawa hati ya ardhi kinyume cha Sheria ya Ardhi ya Mwaka 2004.
Agizo la kuwakamata watumishi hao limetolewa na Mkuu wa Mkoa, John Mongella kutokana na kikao cha dharura alichokiitisha ofisini kwake baina yake na watumishi hao wa idara hizo.
Mongella alisema amewaita ofisini kwake watumishi wote kutoka idara za Ardhi, Mipango Miji na Ujenzi kutaka kujua ni nani alitoa kibali kwa mmiliki wa kiwanja hicho kilichopewa namba 09 L kinachopatikana katika Barabara ya Uganda mjini Bukoba, huku watumishi hao wakionekana kutupiana mpira.
Alisema watumishi hao walikuwa wakitambua kuwa kiwanja husika kipo katika hifadhi ya Mto Kanoni ambao umekuwa ukiathiriwa na ujenzi holela na kuhatarisha uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Victoria.
Kiwanja hicho ambacho kiliguswa na safishasafisha ya Desemba 9, mwaka huu siku ya maadhimisho ya Uhuru ambayo katika mkoa huo yaliambatana na usafi na uondoshaji wa makazi yaliyo ndani ya mita 60 kutoka katika hifadhi ya mto Kanoni unaopeleka maji yake ndani ya Ziwa Victoria.
Ofisa Mipango Miji wa Manispaa ya Bukoba, Catres Rwegasira naye alikuwa na maswali ya kujibu mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Nassor Mnambila na Mkuu wa Mkoa huo.
Rwegasira alisema kwa mujibu wa sheria mpya ya ardhi ya mwaka 2004, hairuhusiwi mtu yeyote kuendesha shughuli wala kuweka jengo katika eneo hilo la mto ndani ya mita 60. Naye Ofisa Msanifu wa Majengo, Abubakar Issa alipohojiwa na mkuu huyo wa mkoa kuhusu nani alitoa kibali cha ujenzi katika kiwanja hicho wakati wakijua kuwa ni makosa; Issa alikubali kuwa yeye ndiye alihusika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Aron Kagulumjuri alisema Manispaa hiyo ilikwishapiga marufuku ujenzi katika kiwanja hicho kinachopakana na mto huo, lakini hajui ni namna gani taratibu zilikiukwa.
Mkuu wa mkoa alisema watumishi hao 15 wamechukuliwa na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Bukoba kwa uchunguzi zaidi na endapo yeyote atabainika na shtaka kujibu hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.
Post a Comment