Header Ads

Kikwete Ajibu Tuhuma Za Kulea Ufisadi Bandarini.......Aitetea Familia Yake, Awapiga Kijembe UKAWA


RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema katika uongozi wake wa miaka 10, hakuwahi kuagiza mtu asamehewe kontena lake lisilipe kodi na angefanya hivyo, mapato ya Serikali yasingeongezeka kutoka Sh bilioni 177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.

Akizungumza baada ya kuwashitukiza wananchi wa Chalinze katika soko kuu la eneo hilo kwa kuungana nao kufanya usafi kuitikia agizo la Rais John Magufuli jana asubuhi, Kikwete alisema katika uongozi wake hakuwahi kuagiza mtu anayestahili kulipa kodi asilipe kodi.

Alisema wakati huu ambao amepumzika baada ya kustaafu, amepata nafasi ya kusoma mitandao na magazeti mbalimbali na kukuta baadhi ya watu, wakimshutumu na kumtukana yeye na familia yake wakimhusisha na ukwepaji kodi.

“Ni afadhali wanishambulie mimi ila wamuache Rais Magufuli (John Pombe) afanye kazi, ni maneno ya walioshindwa wasinilaumu, aliyewashinda ni Magufuli sasa hawana la kusema. Ni sawa na siasa za maji taka, lakini watakuwa wanapoteza muda wao na kufanya kazi bure, kwa kuwa mimi sigombei kitu chochote tena.

“Wanahusisha mpaka na familia yangu, kama mimi mwenyewe sijawahi kuruhusu mtu hata mmoja atoe kontena bila kulipia kodi, siamini kama mke wangu (Mama Salma) au mwanangu Ridhiwani (Mbunge wa Chalinze), wangeweza kufanya hivyo tu na watu wakawasikiliza.

“Wanachonga tu, wengine wamesema Kikwete hachomoki, kwani nimechomeka nini?” Alihoji na kusababisha watu walioshirikiana naye kufanya usafi katika soko hilo kucheka na kuanza kushangilia.

Alisema nafasi ya urais aliyoaminiwa na Watanzania kwa miaka 10, ilikuwa yake na haikuwa na ubia na mkewe wala mtu mwingine yeyote.

Kikwete aliwataka Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli katika jitihada anazofanya za kukabiliana na wakwepa kodi, huku akitoa mfano akisema wakwepa kodi kwa Serikali ni kama inzi na kidonda, hawaondoki bila kufukuzwa na ukiacha kuwafukuza wanarudi.

“Serikali ina wajibu kwa wananchi, wanataka barabara, shule, hospitali ziwe na dawa na mengine mengi, lakini haya yote yanahitaji fedha na Serikali inapata fedha kutoka katika vyanzo vya kodi,” alisema.

Alisema pia yapo mapato mengine ikiwemo ushuru mbalimbali kama katika kulipia leseni, hati za kusafiria na nyingine, lakini pia Serikali inaweza kuchukua mikopo na misaada.

Kikwete alisisitiza kuwa wakati wa uongozi wake, kazi hiyo ya kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ilifanyika, ndio maana alifanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh bilioni 177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.

Pamoja na mafanikio hayo ya uongozi wake, Kikwete alisema bado mahitaji ya Serikali kwa watu wake, yameendelea kuwa makubwa kuliko upatikanaji wa mapato.

“Tunapaswa kuendelea kuboresha mifumo ya kodi, taasisi za mapato na kupata watendaji waadilifu, kwa kuwa kama mifumo na taasisi vikiwa imara, lakini watendaji si waaminifu haisaidii.

Alisema kazi hiyo anayofanya Dk Magufuli ni kubwa kwa kuwa inahusisha kunyang’anya tonge watu na kusisistiza namna bora ya kumuunga mkono ni kulipa kodi na wakusanyaji wa mapato ya Serikali wawe waaminifu.

Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alisema hata katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho walichokaa juzi, waliamua kumuunga mkono Rais Magufuli na kuwataka wanachama wote wa chama hicho kufanya hivyo.

“Ni pale tu mapato yatakapoongezeka, ndipo wajibu wa Serikali katika kuhudumia wananchi utawezekana, tukimuunga mkono Rais wetu mzuri ataweza na mapato yakiongezeka, maji yatapatikana, mapato yakiongezeka, zahanati na hospitali zetu zitapata dawa za kutosha, mapato yakiongezeka barabara za lami zitajengwa,” alisisitiza.

Alisema katika Serikali Kuu, makusanyo yako nyuma ya asilimia 10 ya lengo, lakini kwa juhudi za Rais Magufuli, hali inavyokwenda lengo hilo litapitwa na Serikali itaanza kuzungumzia makusanyo ya matrilioni kwa mwezi.

Hata hivyo, alisema juhudi hizo za Serikali Kuu hazionekani katika halmashauri ambako ni kama hakuna kazi inayofanyika na hata pale kunapokuwa na juhudi za kukusanya mapato, wakati mwingine yanaishia mikononi mwa wajanja.

Kikwete ambaye alifanya usafi katika soko ikiwemo kufagia, kukusanya na kuzoa taka akiwa na mkewe, huku akikataa kuvaa vifaa vya kuzuia vumbi, aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi.

Alisema uamuzi wa Rais Magufuli wa kutumia maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru, kuwataka wananchi wote wafanye usafi, ni wa busara na si wa kukurupuka kwa kuwa mwaka huu taifa lilikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu.


No comments