Acheni kufanyakazi kwa mazoea-Ummy.
SERIKALI imewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kufikia malengo yaliyowekwa. Hatua hiyo inaelezwa itasaidia kurahisisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi kwa kutoa huduma bora na zinazofikiwa kwa wakati.
Akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kila mtumishi wa umma anapaswa kutekeleza kwa bidii Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.
“Sekta ya afya imeingizwa kwenye mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa, ili tuyakifia matokeo makubwa sasa pamoja na mambo mengine tunahitaji kubadilika sana katika utendaji wetu wa kazi,” alisema Mwalimu.
Aidha, Waziri huyo alisema pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika sekta ya afya, Wizara hiyo haina budi kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.
Aliwataka watumishi wa wizara hiyo kutekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa na Rais John Magufuli katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la 11, kwani hotuba yake rasmi ya masuala muhimu yanayopaswa kutekelezwa na kusimamiwa katika kipindi cha miaka mitano.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Donan Mmbando alisema katika kutekeleza mpango wa tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa, Serikali imeainisha maeneo manne ya utekelezaji ili kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi.
Dk Mmbando aliainisha maeneo hayo kuwa ni mgawanyo wa watumishi wa kada ya afya, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, ubora wa huduma na kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto.
HABARI LEO
Post a Comment