UZOEFU,BUSARA KUMBEBA SPIKA.
WABUNGE jana
walianza kujisajili kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11
wiki ijayo, huku wengi wao wakitoa maoni ya sifa wanazozitaka kwa Spika mpya wa
Bunge hilo, zikiwemo uzoefu, busara, kujua kanuni na mwenye utayari wa
kuyakabili mabadiliko.
Pia wabunge
hao wametoa maoni ya kuomba Mungu amuongoze Rais Dk John Magufuli ateue Waziri
Mkuu ambaye atakuwa mfuatiliaji wa mambo na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi
makini. Mbunge wa Kavuu, Dk Pudenciana Kikwembe (CCM) akizungumza alisema ni
muhimu kupata Spika mzoefu, mwenye busara na atakayeweza kutafsiri vyema
kanuni.
“Hili Bunge
litakuwa na changamoto nyingi sana, kuna haja ya kupata mtu atakayeweza kutumia
vyema kanuni, lakini afahamu sheria na awe na uzoefu wa kutosha. “Kwa Waziri
Mkuu, awe na uwezo wa kazi, mfuatiliaji na ambaye ataweza kukabiliana na
changamoto mbalimbali,” alisema mbunge huyo, ambaye awali alikuwa Mbunge wa
Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa.
Mbunge wa
Mpwapwa, George Malima Lubeleje (CCM), ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo hilo kuanzia
mwaka 1990 hadi 2010, kabla ya kurejeshwa tena safari hii, alisema kwa uzoefu
wake anaamini Bunge hilo linahitaji Spika mzoefu, anayejua kanuni na sheria na
asiegemee upande wowote. Kuhusu Waziri Mkuu, alisema anahitajika msomi na
anayeijua vizuri Tanzania, mtendaji na atakayeweza kuendana na kasi ya Rais
Magufuli, huku akitaja sifa ya ziada kwamba ni kujulikana kimataifa.
Mbunge wa
Nzega Vijijini, Dk Hamis Kigwangwala alisema bunge hilo la 11 litakuwa la
vuguvugu, hivyo anahitajika Spika mwenye hekima na anayeweza kukabili
mabadiliko ya wakati. “Ni Bunge la siasa za kazi si siasa za siasa, Spika awe
na busara za kutosha, uzoefu na hekima za kutosha. “Waziri Mkuu mzuri ni yule
atakayeendana na kaulimbiu ya Hapa Kazi tu, ni vizuri akija mtu mpya maana Watanzania
wanataka mabadiliko, hata baraza la mawaziri liwe na sura mpya si mambo ya sura
zilezile zilizozoeleka.
“Huko
mitaani watu wakisikia kuna mabadiliko ya aina fulani tu ya viongozi, kwao hilo
ni furaha tosha, wanataka nao waone utendaji wao,” alisema Dk Kigwangwala
ambaye hii ni awamu yake ya pili. Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema),
alisema suala la uzoefu na kujua sheria ni mambo ya msingi kwa Spika mpya,
lakini lazima awe na uwezo wa kuhimili changamoto za bunge hilo.
“Bunge hili
litakuwa si mchezo, vijana wengi, wa umri wa kati na hata wazee, pia idadi ya
wapinzani imeongezeka sana, kutakuwa na mambo mengi na hili Bunge litakuwa moto
kuliko mabunge yote katika historia ya Tanzania. “Spika wa kuburuza Bunge
hatufai, atakayesikiliza upande fulani tu hatufai, tukimpata Spika atakayeingia
na itikadi za vyama hapatatosha hapa,” alisema Mbunge huyo ambaye hiyo ni mara
ya kwanza kuingia bungeni.
“Kuhusu
Waziri Mkuu, naomba sana Mungu amuongoze Rais apate mtu atakayemsaidia hasa,
mchapakazi na si mlegevu. “Rais ana mambo mengi, sasa tunataka amsaidie, awe
Waziri Mkuu makini, akienda Rais Muhimbili yeye ana uwezo wa kuchukua hatua za
kiufuatiliaji mara moja,” alisema Bilago. Naye Mbunge wa Mikumi, ambaye pia ni
mpya katika bunge hilo, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ alisema kuna changamoto
nyingi na anaamini Bunge la 11 litakuwa la aina yake.
“Namna
nilivyowasikia kaka zangu walionitangulia Tundu Lissu (Mbunge wa Singida
Mashariki) na Joseph Mbilinyi (Mbunge wa Mbeya Mjini), tunahitaji Spika mtenda
haki, mzalendo na ambaye hatayumbishwa na upande wowote. “Kwa Waziri Mkuu
tunahitaji mzalendo, ambaye atakuwa mshauri mzuri sana kwa Rais,” alisema
Haule. Kwa upande wa Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alisema yeyote
atakayepitishwa na CCM atakuwa Spika mzuri na ana imani chama hicho ni makini
katika kufanya uamuzi.
Kwa upande
wa Waziri Mkuu alisema watafurahi wakipata mtu ambaye anaweza kuchukua hatua na
mwenye kufanya utafiti wa kutosha na kumtolea mfano Waziri Mkuu aliyepita,
Mizengo Pinda kwamba alikuwa na busara na hakuwa akikurupuka. Naye Mbunge wa
Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema kwanza sifa kuu ya Spika ni lazima
awe Mbunge kwani itakuwa si jambo jema kuwa na Spika asiyekuwa mbunge.
“Huwezi kuwa
na Mkuu wa Majeshi ambaye si mwanajeshi, ama una mkuu wa Jeshi la Polisi halafu
si askari, lazima Spika awe Mbunge, awe na uzoefu kama kushika nyadhifa
mbalimbali mfano Naibu Spika, au Mwenyekiti wa Bunge. “Kwangu mimi bila
kumung’unya maneno anayefaa kuwa Spika ni Job Ndugai (Mbunge wa Kongwa CCM) na
Naibu Spika ni Mussa Azzan Zungu (Mbunge wa Ilala, CCM). “Ndugai alikuwa Naibu
Spika Bunge la 10, Zungu Mwenyekiti wa Bunge, sifa zinatosha,” alisema mbunge
huyo.
Naye Mbunge
wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), alisema anahitajika Spika
mchapakazi, ambaye hataangalia sura ya mtu bali kazi tu. Kwa upande wake Mbunge
wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alisema ni vyema kupata Spika ambaye
hatafungwa na itikadi za vyama, lakini pia awe na uwezo wa nafasi hiyo. Idadi
kubwa ya wabunge ilijitokeza jana kujisajili ikiwa ni suku ya kwanza tu, ambapo
shughuli ya usajili itaenda hadi kesho.
Waliojitokeza
Katika hatua nyingine, leo ndio mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu kwa
wanachama wa CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika na Naibu Spika
katika Bunge la 11, linalotarajiwa kuanza wiki ijayo, idadi imeongezeka kwa
waombaji na kufikia 22. Akizungumzia uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo,
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Oganaizesheni,
Muhammed Seif Khatib, alisema jana wabunge wawili walijitokeza kuchukua fomu za
nafasi ya Spika na Naibu Spika.
Waliojitokeza
hiyo jana kuchukua fomu ya Spika ni mbunge mteule wa Kasulu Mjini, Daniel
Nsanzugwanko na mbunge mteule wa Ilala, Mussa Azzan Zungu ambaye mpaka jana
alikuwa mgombea pekee wa nafasi ya Naibu Spika na tayari amesharudisha fomu
hiyo. Khatib alisema hadi kufikia hiyo jana idadi ya waliokwishachukua fomu
kuwania kuteuliwa nafasi ya spika kwa CCM, ni wanachama 22.
Akifafanua
shughuli hiyo ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo, Khatib alisema utaratibu
uliowekwa na chama hicho, ulikuwa ni kwamba kwa wanachama ambao si wabunge
wachukue kuanzia Novemba 11 na 12, mwaka huu ili kutoa nafasi fomu zao kwenda
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya uhakiki wa sifa zao. Alisema kwa
mantiki hiyo, upande wao uchukuaji fomu ulikamilika juzi na nafasi iliyopo sasa
ambayo hata hivyo itakoma ifikapo saa kumi jioni leo, ni kwa wabunge wa CCM,
wenye nia ya kuwania nafasi hizo.
“Tumeshafunga
milango kwa wananchama wasio wabunge wanaowania nafasi hizo, na sasa milango
iko wazi tangu jana kwa wabunge wanaotaka nafasi hiyo, ila ifikapo saa kumi
jioni kesho (leo) tutafunga,” alisema Khatib. Alisema baada ya kufunga milango
kwa wanaowania nafasi hizo, kazi iliyobaki ya kuteua wagombea wa nafasi hizo,
itafanywa na Kamati Kuu ya chama hicho, ambayo hata hivyo hakusema itakaa lini
kuamua.
Majina
Waliokwishachukua fomu kuwania nafasi ya Spika ni pamoja na aliyekuwa Naibu
Spika katika Bunge la 10 na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Arkson na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Dk Didas Masaburi.
Wengine ni
Spika mstaafu, Samuel Sitta, Mbunge mteule wa Chato, Dk Medard Kalemani, Diwani
wa Goba - Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius Pawatila, Agnes Makune na
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa zamani wa
Afrika Mashariki, George Nangale, Simon Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda.
Pia yumo aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu
mwenye umri wa miaka 28, Veraikunda Urio.
Kadhalika
yupo aliyekuwa mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na aliyekuwa mmoja wa
wagombea 42, waliojitokeza kuwania nafasi ya urais ndani ya CCM katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu, Dk Kalokola Muzzamil.
Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Songea Mjini, Dk
Emmanuel Nchimbi, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, Philip Marmo na Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia,
Profesa Costa Mahalu.
CHANZO: HABARI LEO.
Post a Comment