Header Ads

Vifaa Kama BVR Vyanaswa Vikiandikisha watu Jijini Dar..


Hofu ilitanda jana katika kiwanda cha MM Steel cha jijini Dar es Salaam, baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa mashine ya kusajili wapigakura kwa mfumo wa elektroniki (BVR) inatumika kuandikisha wafanyakazi katika kiwanda hicho.

Kutokana na hofu hiyo, baadhi ya maofisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na Mwanasheria wa chama hicho, John Mallya, Polisi na Tume Taifa ya Uchaguzi (Nec), walifika kiwandani humo na kufanya upekuzi ikiwamo kuondoka na baadhi ya vifaa vilivyokuwa vinatumika.

Baada ya kukubaliana pande zote, vifaa hivyo ambavyo ni vya kuchukua alama za mikono, macho, scanner na kompyuta mpakato, vilichukuliwa na Polisi ili baadaye vikakabidhiwe Nec.

Polisi, Chadema na Tume, walielezwa na Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo, Abubakari Mlawa, kuwa kampuni hiyo imeamua kuandikisha wafanyakazi wake kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi katika viwanda saba walivyonavyo na kushindwa kuwatambua wafanyakazi.

“Tunaendesha zoezi la kuweka ‘data base’ kwa ajili ya wafanyakazi wetu wote kwa maana ya kupiga picha na kuandika taarifa zake zote; amezaliwa wapi, amesoma wapi na ameanza kazi lini, wakati tunaendelea na zoezi letu walikuja watu wakajitambulisha kuwa ni polisi wakawaweka chini ya ulinzi watu wanaofanya zoezi hilo. Tulipowauliza ni kina nani, walisema wanatoka Chadema na wamepewa taarifa kuwa tunatoa vitambulisho vya kupigiakura,” alisema na kuongeza:

"Ili tujiridhishe, tuliamua kuwaita Nec na polisi kuthibitisha wamechukua mashine kwenda kujiridhisha. Tunafanya zoezi hili wiki nzima na tumeandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 na tuna zaidi ya wafanyakazi 900.”

Hata hivyo, wakati anahojiwa na Polisi na Chadema kama kifaa cha alama za vidole wametoa wapi, Meneja huyo alisema walitoa zabuni kwa kampuni ambayo hakuitaja na alipotakiwa kuitaja hakufanya hivyo.

Afisa wa ICT wa Nec, Amosi Madaha, akizungumza mara baada ya kufika na kulinganisha mashine ya alama za vidole ya Nec na yao, alisema ni mapema sana kueleza kama vifaa hivyo ni sehemu ya vifaa vya BVR hadi watakapokwenda kuvichunguza zaidi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa Nec, Salvisius Mkwera, alisema walipata taarifa kuna uandikishaji wa wapigakura unafanyika ndani ya kiwanda hicho na walipofika walikuta baadhi ya vifaa ambavyo ni ngumu kusema.

“Tulichokiona ni baadhi ya vifaa ambavyo vinafanana na vifaa vya Tume, lakini hatuwezi kuhakikisha kama ni vyetu au siyo, tulichokubaliana na polisi ni kuchukua vifaa hivyo vifanyiwe uchunguzi zaidi tujiridhishe na vifaa tulivyonavyo,” alisema.

Alitaja kifaa kinachofanana na cha Nec kuwa ni `finger print machine,' lakini wamechukua na vifaa vingine kama kompyuta mpakato na scanner.

Alisema pia wataingia kwenye data base ya kampuni hiyo ili kujiridhisha na taarifa zilizoingizwa.

Alisema pia wamechukua orodha ya wafanyakazi waliorodheshwa kwenye karatasi ili kuangalia kwenye daftari la kudumu la wapigakura kama kuna uwiano wowote.

“Tutatoa taarifa mapema na kwa wakati ili kuondoa wingu lililotanda kwa sasa, tunataka pande zote zijiridhishe hivyo tutafanya kwa uwazi kueleza kama hizi ni mashine zetu,” alisema.

Baadhi ya wafanyakazi ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema wameshtushwa na uandikishaji huyo kwa kuwa unafanana na BVR hasa kwenye uchukuaji wa alama na kuamua kutoa taarifa.

No comments