Header Ads

UKAWA WAPONDWA.

MUUNGANO wa vyama vinne vinavyoshirikiana katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umejikuta ukikumbana na upinzani unaoshika kasi nje ya muungano huo, wakati ukikabiliana na sintofahamu inayoendelea ndani yake, huku viongozi wake wakilalamika kuhujumiana wenyewe kwa wenyewe.
Jana, Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Hamphrey Polepole, badala ya kuunga mkono umoja huo unaojinasibu kutetea Rasimu ya Katiba iliyotengenezwa na Tume hiyo, alielezea kushangazwa na Chadema kukubali kuondoka kwa misingi ya kupambana na rushwa, na kumtangaza mgombea urais, ambaye kilimtuhumu kwa kadhia hiyo.
Mbali na Polepole, Kiongozi Mkuu wa ACT –Wazalendo, Kabwe Zitto, akizungumza mkoani Morogoro, alitaka Watanzania waunge mkono wagombea wa chama hicho, kwa madai kuwa vyama vinavyounda Ukawa, vimebadilika ghafla kutoka kuwa mstari wa mbele kutetea wanyonge na kugeuka kukumbatia ufisadi, huku CCM ikituhumu umoja huo kwa kughushi kadi zake.
Polepole Akizungumza kupitia kipindi cha ‘Mada Moto’ kilichorushwa hewani na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten juzi usiku, Polepole alisema chama hicho hakikupaswa kukimbilia kumpokea Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kwa kuwa kilitumia kete ya umaarufu wake kisiasa kumshutumu kuwa hafai.
Alisema, Chadema ni taasisi ambayo ina misingi yake, hakuna mtu anayepaswa kuivuruga kwa nia ya kutaka kumfanya mtu mmoja anufaike na chama hicho.
“Chadema wana misingi yao ambayo hakuna mtu anayepaswa kuivuruga. Kwa maana nyingine misingi hiyo ni sawa na imani ambayo haibadiliki kutoka katika msingi wake, hivyo walichofanya nawashangaa,” alisema.
Mjumbe huyo wa Tume hiyo ambayo ilikuwa chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu, Joseph Warioba, alisema hata upande wa Lowassa na wana Chadema wanapaswa kujiuliza iwapo ujio wake ndani ya chama hicho una manufaa mapana yenye malengo ya kuendeleza misingi iliyowekwa au wanafikiria kushika dola pekee.
Alisema waziri mkuu huyo wa zamani amekaribishwa Chadema ambacho kinaunda Ukawa, akiwa tayari ameshiriki kuiunga mkono na kuipitisha Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi, wakati Ukawa wenyewe wanaipinga, hivyo kilichompeleka ni msukumo wa kuingia madarakani na siyo Katiba inayotetewa na umoja huo.
Alihoji kama kweli kifikra mgombea huyo anarandana na mawazo ya wale waliomkaribisha, wakati wao wamekuwa wakihubiri kile kilichomo ndani ya Katiba Iliyopendekezwa na Tume, ambayo msimamo wake ni serikali tatu wakati Lowassa alipiga kura na kuunga mkono uwepo wa serikali mbili.
“Ukisikiliza wanasema tunataka kuing’oa CCM, hiyo ndio mada kubwa. Huyu ndio anaijua CCM, mimi nauliza hivi sisi tuna mtindo wetu wa kufikiri, tuna mtindo wa kufanya mambo yetu ili yaende? Hivi leo mnampata mtu mwingine ana itikadi nyingine anakuja, kiitikadi hilo haliwezekani. “Hivi unadhani Ukawa ina uhalali wa kusema inapambana na ufisadi ilhali inafahamu Lowassa, Membe na wengine walisimamishwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kufanya rafu? Hivi ninyi mna uhalali leo tena wa kumyooshea mtu kidole?” Alihoji.
Alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ana siri nzito moyoni kwa kuwa haiwezekani kiongozi huyo kuwa miongoni mwa waliomkaribisha Lowassa na siku chache akaamua kujiondoa kabisa madarakani.
“Mimi nasema, na nataka niwaambie waandishi wa habari mheshimiwa Lipumba ana siri kubwa...”alisema mjumbe huyo ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa nchini.
Zitto Naye
Zitto akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu Jimbo la Morogoro Mjini, mkoani humo juzi aliwaomba Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa wa Morogoro kuunga mkono chama chake kwa kuchagua madiwani, wabunge na rais ili kipate uwakilishi kwa lengo la kuwatetea watu wanyonge.
Alisema ACT-Wazalendo, ndio chama kilichobaki katika kuendelea na misingi yake imara ya kutetea wanyonge, baada ya kutokea mtikisiko wa vyama vya siasa vya upinzani, hasa vinavyounda Ukawa.
Kwa mujibu wa Zitto, vyama hivyo vya Ukawa vimebadilika ghafla kutoka mstari wa mbele wa kutetea watu wanyonge, na kugeuka kukumbatia ufisadi, kinyume na msimamo wao wa awali na matarajio ya wananchi walio wengi.
“Ndugu wananchi wa manispaa ya Morogoro, chama hiki sasa ndiyo kimbilio lenu, hakijabadili misingi yake iliyojiwekea ya kupambana na ufisadi... Tunalo azimio la Tabora tulilohuisha kutokana na Azimio la Arusha na moja ni kila kiongozi lazima atangaze kwa kuorodhesha mali yake,” alisema Zitto.
Kadi za CCM
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amedai kuwa chama hicho kimebaini mchezo mchafu unaotaka kufanywa na Ukawa wa kutengeneza kadi bandia za chama hicho na kuzigawa kwa watu wao, ili baadaye asipopita mgombea wao, ionekane wana CCM wanakihama chama kwa kurudisha kadi zao.
Akizungumza katika Makao Makuu ya CCM, mjini Dodoma jana, Nape alisema kuna taarifa za uhakika kuwa kuna baadhi ya makundi ya Ukawa yamepanga mchezo huo wa kutengeza kadi bandia.
“Wameanza kuratibu mchezo huo ili wazigawe kadi hizo kwa watu wao, ili baadaye asipopita mgombea wao, ionekane wana CCM wanakihama chama chao kwa kurudisha kadi hizo kwenye shughuli mbalimbali za vyama hivyo vinavyounda Ukawa. “Wakati tunachunguza kwa kina suala hilo, Ukawa waache mchezo huo wa ovyo na Watanzania wakwepe mchezo huo na wawe makini,” alisema.
Lipumba ‘msaliti’
Wakati huo huo, vyama vinavyounda Ukawa, vimeonesha kuchukizwa na hatua ya aliyekuwa Mwenyekiti mwenza wa Ukawa na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Lipumba kujiuzulu wadhifa wake ndani ya chama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema pamoja na Profesa Lipumba kung’atuka madarakani, bado Ukawa itaendelea na harakati za kwenda Ikulu.
“Tunasema aende aendako, sisi Ukawa tunaendeleza harakati za kuelekea Ikulu, hata kama Profesa Lipumba ameamua kuondoka wakati safari imeanza, hii inaonesha alikuwa hataki Ukawa tuingie Ikulu,” alisema Mwalimu.
Alisema si busara kwa uamuzi alioufanya Profesa Lipumba, kwani akiwa Mwenyekiti Mwenza, hakupaswa kufanya hayo wakati akijua kwamba hiyo ilikuwa safari ya pamoja. Alisema wameshangaa mwenzao ameamua kuwageuka katikati ya safari.
“Hayo madai ya kwamba Ukawa imepokea wanachama wa CCM, ambao waliipinga Rasimu ya Jaji Warioba, hayana mashiko. “Hata hayo makubaliano anayosema Ukawa tulikubaliana, awaoneshe, sisi hatujakubaliana chochote, yeye ana sababu zake za kuondoka, ndiyo aziseme”, alisisitiza Mwalimu.
Alisema Ukawa iko imara, ndio maana jana wamefanya mkutano na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chama cha NCCRMageuzi kuonesha dhamira yao ya kweli ya kushikamana.

Mwalimu alisema katika safari hiyo ya kwenda Ikulu, wao wamejipanga na wataendelea na safari hiyo kwani Ukawa bila Lipumba ipo na vyama vyote vinavyounda umoja huo vinaendelea na mchakato huo. Umoja huo unaundwa na vyama vinne ambavyo ni CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.HABARI LEO

No comments