Header Ads

SUMAYE:NIMEJIVUA WA CCM NA KUJIUNGA UKAWA ILI KUONGEZA NGUVU YA MAGEUZI ITAKAYOSAIDIA KUING'OA CCM.


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ametangaza rasmi kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga kwenye vuguvugu la mabadiliko kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Sumaye ametangaza uamuzi huo leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Legde Plaza uliopo katika Hoteli ya Bahari Beach Jijini Dar es Salaam.

“Leo nimeamua kuondoka CCM na kujiunga na UKAWA, uamuzi huu haukuwa rahisi katika familia yangu…, suala la kujiunga na chama gani itajulikana baadaye,” amesema.

Amesema, atasaidiana na Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chadema na pia mwakilishi wa UKAWA kufanikisha mageuzi.

UKAWA unaundwa na vyama vinne vya upinzani ambavyo ni Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na NLD.

Sumaye amesema, Lowassa amekaa kwenye nafasi mbalimbali za utawala ndani ya serikali hivyo anastahili nafasi hiyo na kwamba, hana tatizo na utendaji wa mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Mgufuli lakini sio katika ngazi ya urais.

“Sina tatizo na Magufuli, naamini hakuhonga na ni mchapakazi lakini ana mapungufu mengi katika nafasi hiyo (urais),” amesema.

Mkutano huo wa Sumaye na waandishi wa habari pia umehudhuriwa na Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Siasa na Bunge wa CUF, Shaweji Mketo na viongozi wengine wa UKAWA.

Tayari Lowassa na mgombea mwenza wake Juma Duni Haji jana wamerudisha fumu za kugombea urais kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) na kukidhi vigizo vilivyowekwa.

Hatua ya Sumaye kuhama CCM inakuja ikiwa ni siku moja kabla ya Dk. Magufuli kufungua rasmi kampeni ya chama chake kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Kwenye mkutano huo Sumaye ambaye aliongozana na mkewe Esther Sumaye pamoja na wana familia wengine amesema, anaondoka kwenye chama hicho ili kuongeza nguvu ya upinzani.

“Siji upinzani kufuata cheo, nakuja kuimarisha nguvu. Sijadai cheo wala fedha. Nipo tayari kusaidia upinzani ili uwe na nguvu,” amesema Sumaye na kuongeza:

“CCM imezubaa, inajifanya itashinda. Wananchi wanataka mabadiliko na hatuwezi kuwaacha hivi hivi, sisi wenye uchungu na nchi hii hatuwezi kuwaacha hivi hivi. Nimekuja huku ili kuongeza nguvu ya mabadiliko.”

Hata hivyo Sumaye amewataka wanachama wa CCM pamoja na watumishi wa serikali walio tayari pia wajiunge na UKAWA ili kuhakikisha wimbi la mageuzi linafanikiwa.

“Mimi sijui kama ni mmoja wa wale walioitwa makapi, ningejua ningetoka mapema…, sitoki CCM kwa hasira ya kutoteuliwa, kumchukia mgombea urais wa CCM, kuchukia uongozi wa juu wala kudhoofisha CCM, badala yake natoka ili kuimarisha CCM,” amesema.

Akifafanua kauli hiyo amesema kuondoka kwake CCM na kuimarisha nguvu ya UKAWA kutaisaidia CCM kutolala na kuongeza nguvu ili kupambana na vyama vya upinzani.

Amesema, wana CCM hawapaswi kusikitika kwa yeye kuhama chama hicho kwani ni mtu wa kawaida ndani ya chama hicho na kwamba, hana cheo chochote.

“Wana CCM hawana sababu ya kulalamika, mimi ni sisimizi ndani ya CCM, sina nafasi yoyote hata ujumbe wa tawi,” amesema na kuongeza, chama hicho hakikuona umuhimu wake na pengine kitauona baadaye.

Hata hivyo Sumaye amesema, hakuhama kwa sababu ya kumfuata Lowassa kwa kuwa, ametoka Kaskazini, “lakini pia si kwa sababu Mbowe ni mtu wa Kaskazini,” isipokuwa ni kuimarisha mageuzi.

Hata hivyo ameoneshwa kutishwa na wimbi la mageuzi nchini na kusema “wimbi hili kulizuia si kazi rahisi.”

Sumaye ameshutumu vikali hatua ya wachache kuharibu taratibu za CCM katika kupata mgombea urais kupitia chama hicho na kuwa, alijua mapema kwamba jina lake halitafika mbali.

Anasema, hana tatizo na mfumo wa kupata wagombea isipokuwa tabia ya watu wachache kwenda na majina ya wagombea kinyume na taratibu za chama.

“Katika mfumo huu mtu mwenye nafasi ya juu na anataka akuingize anaweza kufanya hivyo na kama hataki anakuondoa. Mfumo huu ni mbuvu, safari haya yametokea sana.

“Rais, katibu mkuu hana nafasi ya kuweka mgombea. Rushwa ni tatizo ndani ya CCM, ukipinga rushwa unaonekana tatizo ndani ya CCM. Hili linathibitika,” amesema.

Hata hivyo ameshauri wale walio na mtazamo kwamba, nje ya CCM hakuna maisha ya siasa wabadilike  maana mawazo hayo yamepitwa na wakati.

No comments