PRESHA YA UBUNGE CCM YAPANDA.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza kurudiwa kwa kura za maoni kesho katika majimbo matano nchini, kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza wakati wa mchakato wa upigaji kura hizo.
Wakati agizo hilo likitolewa kwa majimbo husika, hatma ya watakaopeperusha bendera ya CCM katika ubunge, udiwani na Wawakilishi inatarajiwa kujulikana wakati wowote kuanzia sasa baada ya vikao vya chama kuanza vikao vyake mjini Dodoma jana.
Kamati Kuu ya chama hicho, ambacho kimesema kipo vizuri na kwamba vikao vyake vya kupata wagombea vinakwenda vizuri, ilitoa jana maagizo ya kurudiwa uchaguzi huo baada ya Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kufungua kikao hicho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kwamba majimbo yaliyokumbwa na dosari hizo na ambayo yanatakiwa kurudia uchaguzi kesho ni Rufiji mkoa wa Pwani, Kilolo mkoa wa Iringa, Makete mkoa wa Njombe, Busega mkoa wa Simiyu na Ukonga mkoa wa Dar es Salaam.
Akitoa maelekezo hayo ya chama, alisema kikao cha Kamati ya Maadili kilimalizika juzi usiku na kwamba jana kikao cha Kamati Kuu kilianza. Alisema kama kitakuwa kimefanikiwa kumaliza, leo kitaanza kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
“Majimbo matano yanatakiwa kurudia kura za maoni Alhamisi Agosti 13 baada ya kutokea dosari mbalimbali...baada ya marudio ya kura hizo yanatakiwa kuleta matokeo kwa ajili ya uamuzi,” alisema.
Nape alisisitiza kwamba kazi ya kupata wagombea wa nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani inaendelea vizuri. Hata hivyo, hakuainisha dosari zilijitokeza katika majimbo hayo matano, kiasi cha kuamua kurudia kura.
Busega
Katika Jimbo la Busega, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani alitangazwa kuangushwa kwenye kura za maoni baada ya kupata kura 11,829 wakati Dk Raphael Chegeni aliongoza kwa kupata kura 13,048. Hata hivyo, matokeo hayo yalipingwa kwa madai ya kugubikwa na uchakachuaji.
Chegeni aliwahi kuwa mbunge kabla ya Dk Kamani, ambaye ndiye mbunge wa sasa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu.
Ukonga
Kwa upande wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa ndiye alikuwa ametangazwa kuongoza kwa kupata kura 10,000 akifuatiwa na Ramesh Patel aliyejipatia kura 7,356. Jimbo hilo lilikuwa na wagombea 13. Silaa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na ni Meya wa Ilala.
Kilolo
Venance Mwamoto ni mgombea aliyekuwa ameibuka na ushindi katika jimbo la Kilolo na kupata kupata kura 11,200 na kufuatiwa na Profesa Peter Msolla aliyepata kura 10,014. Wagombea walikuwa 15.
Akizungumza jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Clement Mponzi alisema uchaguzi huo unarudiwa katika kata zote kumaliza utata uliothibitishwa katika malalamiko yaliyotolewa kupitia rufani ya Profesa Msolla.
Profesa Msolla katika rufaa yake, alisema anapinga matokeo hayo kwa sababu yalitangazwa bila kuridhiwa na wagombea au mawakala wao huku akidai alikuwa anaongoza kwa kura 13,409.
Msolla aliwahi kuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na ndiye mbunge wa sasa wakati Mwamoto aliwahi kuwa mbunge kabla ya Msolla.
Akizungumzia dosari zilizosababisha uchaguzi kurudiwa, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema kuna baadhi ya wagombea hawakuridhika na matokeo hivyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama, ndiyo maana imeamriwa kurudiwa kila mmoja apate haki anayostahili.
Makete
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Bilinith Mahenge anayetetea nafasi yake, alikuwa ameibuka mshindi kwenye kura za maoni kwa kupata kura 8,534 dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Dk Norman Sigala aliyepata kura 8,211.
Wagombea wengine na kura kwenye mabano ni Bonic Muhami ( 500), Fabianus Mkingwa ( 466) na Lufunyo Rafael aliyepata 226.
Rufiji
Kwa upande wa matokeo ya Rufiji, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, alionekana kuanguka kwa kupata kura 3,000 wakati mpinzani wake Mohamed Mchengelwa alipata kura 4,000.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Kaimu Katibu Mkuu wa CCM mkoa wa Pwani , Abihudi Shilla alisema kulikuwa na mkanganyiko wa matokeo hali iliyolazimu wasubiri uamuzi kutoka ngazi ya taifa.
Mbivu, mbichi
Awali akifungua kikao cha Kamati Kuu(CC), Rais Kikwete alisema wanatarajia kufanya kazi jana na leo, kupata watakaopitishwa kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.
“Mkutano umefunguliwa tutafanya kazi leo(jana) na kesho(leo) tupate wataopeperusha bendera, na baada ya kitakachobakia ni CCM iyena iyena mpaka mwisho,” alisema Rais Kikwete.
Aidha, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimkaribisha Mwenyekiti kufungua kikao hicho, alisema wajumbe waliotakiwa kuhudhuria mkutano huo ni 32, lakini waliokuwepo wakati kikao kikifunguliwa ni 25 na kwamba akidi imetimia.
Wajumbe waliohudhuria katika kikao hicho ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri Mkuu Mizengo Pinga, Waziri Mkuu mstaafu Dk Salim Ahmed Salim, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro na Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samiha Suluhu Hassan.
Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wasira, Waziri wa Ardhi, William Lukuvi na Waziri wa Ulinzi Dk Hussein Ali Mwinyi.
Wajumbe wengine ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Makame Mbarawa, wabunge wa kuteuliwa, Zakhia Meghji na Shamsi Vuai Nahodha; Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib, Makamu wa Mwenyekiti CCM, Phillip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Kinana.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar Vuai Ali Vuai, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, Emmanuel Nchimbi, Meya wa Manispaa Ilala, Jerry Silaa na Hadija Abood.
Wajumbe ambao hawakuwepo wakati wa ufunguzi wa kikao hicho ni Makamu wa Rais, Dk Mohammed Ghalib Bilal na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama.
Walioshindwa maoni Wakati huo huo, katika maeneo ya Makao Makuu ya CCM Dodoma, makada mbalimbali wa chama hicho wamekuwa wakiingia na kutoka. Wengine , wakiwamo walioanguka kwenye kura za maoni, walionekana wakiwa wamesimama kwenye viwanja vya ofisi hizo, wakibadilishana mawazo.HABARI LEO
Post a Comment