Header Ads

MGODI WA ACACIA WAAMRIWA KUWALIPA WANAKIJIJI FIDIA.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson mpesya.

SERIKALI kupitia Baraza la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) imethibitisha kuwa maji yaliyotiririka kutoka moja ya mabwawa ya maji katika mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu yalikuwa na sumu.
Akizungumza kwa niaba ya NEMC, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema maji hayo yalipasua moja ya mabwawa yanayohifadhi sumu kali aina ya Synide na kisha kuingia katika kijiji cha namba tisa.
Kijiji hicho kipo katika kata ya Kokala, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga ambapo tukio hilo lilitokea mapema mwezi Januari mwaka huu na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye mazao, vyanzo vya maji pamoja na mifugo.
Kutokana na tukio hilo, serikali ya wilaya ya Kahama kupitia mkuu huyo wa wilaya ilisitisha shughuli za kilimo pamoja kuzuia wananchi wa kijiji hicho kutumia maji ya visima hadi hapo baraza la hifadhi ya mazingira nchini litakapotoa majibu baada ya kufanya uchunguzi.
Alisema kuwa baada ya NEMC kufanya uchunguzi waligundua kuwa sumu iliyomwagika katika kijiji hicho ilikuwa na kiwango cha 1.126 PPM, kiwango ambacho ni kikubwa na kuitaka kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi huo wa Bulyanhulu kuhakikisha kuwa inawafidia wananchi wa maeneo hayo ili wakanunue chakula baada ya kukaa muda wa miezi nane bila ya kujishughulisha na kilimo.
Kwa mujibu wa Mpesya, Sheria ya Udhibiti wa Hifadhi ya Mzingira ya namba 191, kifungu cha 197 kipengele cha namba moja hadi namba nne kinasema kutiririsha maji ya sumu katika makazi ya wananchi ni kosa.
Wananchi wa kijiji cha namba tisa, kata ya Kakola wakizungumza na waandishi wa habari walisema kutokana na sumu hiyo kuingia katika mashamba yao, wameiomba Serikali kuhakikisha kuwa wanalipwa fidia zao kwani kwa kipindi kirefu wamekaa bila ya kufanya shughuli zozote za kimaendeleo, hali iliyowaathiri kiuchumi.
Mmoja wa wananchi hao, Mayunga Peter alitoa lawama kwa mgodi huo kwa kushindwa kuwapa huduma kwa kipindi chote cha miezi minane ingawa eneo hilo la kijiji lipo ndani ya leseni ya mwekezaji na kuongeza kuwa kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa kama ya kuumwa kichwa pamoja na miguu kutokana na kuathirika na kemikali hiyo.HABARI LEO.

No comments