Header Ads

Kura za Maoni CCM: Mawaziri Watano Waanguka.......Yumo Chikawe,Sillima,Mahanga na Makalla.......Aden Rage Pia Kaanguka!!

Matokeo ya awali ya kura za maoni kwa wagombea udiwani na ubunge kupitia chama tawala, yameanza kuanikwa, huku yakionesha kuwa baadhi ya mawaziri, wabunge na watendaji katika chama na serikali wameangushwa.


Kwa mujibu wa matokeo ambayo mtandao huu umeyapata, kwa upande wa mawaziri walioshindwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
 
 Hayo yamethibitishwa na Katibu wa CCM mkoa wa Lindi, Adelina Gefi aliyesema kura za Chikawe katika jimbo lake la Nachingwea alikokuwa anatetea kiti chake, hazikutosha mbele ya Hassan Masalla, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero aliyepata kura 6,444. Chikawe amepata kura 5,128.
 
Wakati Chikawe, mmoja wa wanasiasa mahiri na mwanasheria aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora na pia Waziri wa Katiba na Sheria akikwama katika mchakato wa kurejea bungeni, naibu wake katika Wizara wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima naye ameanguka katika kura za maoni huko jimbo la Bumbwini, Unguja.

Mwanasiasa mwingine aliyekwama katika kura za maoni ni Mahadhi Juma Mahadhi ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 
Mahadhi ameanguka katika kura za maoni katika Jimbo la Paje, Unguja huku mshindi akiibuka kuwa Jaffar Sanya Jussa.
 
Mambo yamekuwa mabaya pia kwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima ambaye ameripotiwa kuanguka katika kura za maoni katija Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani.

Hali kama hiyo imemkuta Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Makongoro Mahanga ambaye ndani ya saa 24 tangu ashindwe kura za maoni katika jimbo alilokuwa analitumikia la Segerea katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, jana alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema.

Katika Jimbo la Mvomero mkoani Morogoro, habari zinasema aliyewahi kuwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Suleiman Saddiq `Murad’ amefanikiwa kumwangusha mshindani wake wa siku nyingi, Amos Makalla ambaye alilitwaa jimbo hilo mwaka 2010 na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, akianzia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Maji ambako yupo mpaka sasa.

Ingawa Katibu wa CCM wa wilaya ya Mvomero, Amos Shimba hakuthibitisha hilo, akisema kwa kiasi kikubwa matokeo yamepatikana, isipokuwa katika baadhi ya maeneo, hivyo matokeo rasmi yatatangazwa leo, tayari kambi za Murad na Makalla zilithibitisha matokeo ya kura za maoni katika jimbo hilo, kwamba hali ya Makalla haikuwa nzuri katika kura hizo.
 
Mshtuko mwingine wa kisiasa umesikika katika Jimbo la Uzini ambako mwanasiasa nguli aliyepata kuwa waziri katika wizara mbalimbali za Serikali ya Muungano, Muhammed Seif Khatib ameshindwa katika kura za maoni.
 
Khatib ambaye kwa sasa ni Katibu wa Oganaizesheni ya CCM, amepata kura 1,333 dhidi ya mpinzani wake, Salum Mwinyi Rehani aliyepata kura 1,521.

Khatib amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20 na katika kipindi hicho alikuwa waziri wa wizara mbalimbali zikiwemo Habari na ile ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Rage `out’, Adadi, Nape safi
Ukiachilia mbali mawaziri hao, baadhi ya wabunge wamekuwa na wakati mgumu majimboni kwao, akiwemo Ismail Aden Rage wa Tabora Mjini. Aidha, Zainabu Kawawa, binti wa Waziri Mkuu wa zamani, Rashid Mfaume Kawawa hakufua dafu mbele ya Mbunge wa Jimbo la Liwale, Faith Mitambo.

Awali, Zainabu alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM.
 
Mbunge mwingine aliyeshindwa katika kura za maoni ni Mtutura Abdalla wa Tunduru Kusini, kama ilivyokuwa kwa wabunge watatu wa mkoa wa Tanga, Herbert Mntanga wa Jimbo la Muheza aliyeangushwa na Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Zimbabwe, Adadi Rajab ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI).

Saleh Pamba, Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Maliasili ambaye anamalizia ubunge wake katika Jimbo la Pangani, amethibitika kukwama mbele ya Jumaa Awesso, kwa mujibu wa Katibu wa CCM mkoa wa Tanga, Shija Othman.

Mbunge wa Korogwe Mjini, Yussuf Nasri naye kura zake hazikutosha, baada ya wanachama wa CCM kumpa kura nyingi Mary Chatanda kuwa ndiye chaguo lao katika kura za maoni ya ubunge.
 
Naye Gregory Teu, Mbunge wa Mpwapwa aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, ameripotiwa kuanguka na mbunge wa zamani wa Jimbo hilo, George Malima Lubeleje.

Katia Jimbo la Kilombero, Abdul Mteketa amegota mbele ya Abubakar Asenga, wakati katika Jimbo la Igalula mkoani Tabora, Naibu Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Athuman Mfutakamba anaburuzana na Mussa Ntimizi, ambapo kufikia jana Ntimizi alikuwa na zaidi ya kura 75,000 dhidi ya 3,400 za Mfutakamba.

Kibamba ni Dk Mukangara
Kwa upande wa baadhi ya majimbo ya Dar es Salaam, walioshinda kwa upande wa CCM ni pamoja na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara aliyeshinda kura za maoni katika jimbo jipya la Kibamba lililogawanywa kutoka jimbo la Ubungo, huku Ramesh Patel aking’ara Jimbo la Ukonga alikowabwaga washindani kadhaa, akiwemo Meya wa Manispaa wa Ilala, Jerry Silaa.

Katika jimbo la Ubungo, kura zimempa nafasi Meya wa Jiji la Dar es Salaam, wakati Abbas Mtemvu ameshinda katika jimbo la Temeke analoliongoza tangu mwaka 2005.
 
Nape apeta Mtama
Nako katika Jimbo la Mtama lililoongozwa kwa miaka 15 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kabla ya mwaka huu kujitosa katika mbio za urais, kijiti kinaelekea kumwangukia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye aliyewabwaga washindani wake kadhaa, akiwemo Suleiman Mathew aliyekuwa Diwani wa Kata ya Vijibweni, Kigamboni

No comments