Header Ads

YANGA, AZAM HAPATOSHI LEO.

Image result for YANGAImage result for AZAM

YANGA na Azam zinakutana leo kwenye mechi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mechi hiyo ni kama marudio ya fainali za mwaka 2012 iliyofanyika kwenye uwanja huohuo wa taifa, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mechi ya leo inatazamwa kwa hisia tofauti ikitarajiwa kuwa ya vuta nikuvute kutokana na uimara wa timu zinazokutana.
Yanga imekuwa ikiisumbua Azam FC mara kadhaa kila inapokutana nayo.
Mara ya mwisho Yanga kuifunga Azam ilikuwa ni kwenye mechi ya ngao ya jamii Agosti mwaka jana, ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Kwenye Ligi Kuu msimu uliopita timu hizo hazikutambiana, ambapo katika mechi ya kwanza zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na mechi ya pili zilitoka sare ya 1-1.
Timu hizo zilimaliza nafasi mbili za juu kwenye ligi hiyo, Yanga ikitwaa ubingwa na Azam ikishika nafasi ya pili.
Kwa sasa timu hizo zimefanya usajili kujiandaa na michuano mbalimbali na hakuna ubishi kwamba kila timu ina kikosi imara, hali inayofanya mechi ya leo kushindwa kutabirika kirahisi.
Akizungumzia mechi hiyo kocha wa Yanga, Hans Van der Pluijm amesema anatarajia kupata upinzani mkubwa kutokana uimara wa wapinzani wake. Hatahivyo, alisema hilo halimtishi kwani hata yeye ana kikosi kizuri ambacho anatarajia kitapata matokeo mazuri leo.
“Mechi yetu na Azam nafahamu itakuwa ngumu sana kwasababu wapinzani wetu nao wana timu nzuri, lakini hatuiogopi kwani hata sisi timu yetu nzuri naamini wachezaji watatupa matokeo mazuri leo,” alisema.
Naye kocha wa Azam Stewart Hall alisema amewaandaa wachezaji wake kuifunga Yanga na hawaiog opi kama wengi wanavyodhani. “Hatuiogopi Yanga, tunao uwezo wa kuifunga na tunaamini hilo litatokea,” alisema.
Chini ya Hall kwenye michuano hiyo, Azam imecheza mechi tatu na kufunga mabao manane huku ukuta wake ukiwa haujaruhusu bao hata moja, matokeo ambayo yanaipa kiburi timu hiyo kuona kwamba hata leo Yanga inaweza isione ‘ndani’.
Kabla ya mechi hiyo ya wenyeji itakayochezwa saa 10 jioni, mechi ya awali itakuwa ni kati ya KCCA ya Uganda dhidi ya Al Shandy ya Sudan.HABARI LEO

No comments