Picha: Diamond awashukuru watanzania kwa ushindi wa tuzo ya MTV MAMA.
Mshindi wa tuzo ya mtumbuzaji bora wa Afrika kwa muziki wa MTV MAMA, Nasib Abdul aka Diamond Platnumz amewashukuru watanzania kwa kumwezesha kupata tuzo ya mtumbuizaji bora wa Afrika huku akiwataka wasanii wa Tanzania kuungana kwa pamoja ili kuufikisha muziki mbali zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika hoteli ya Tansoma jijini Dar es salaam, Diamond aliwashukuru watanzania kwa kuendelea kuunga mkono muziki wake, hali inayoleta heshima kwa Tanzania.
“Kwanza nawashukuru kampuni ya Tigo kwa kuniwezesha kukutana na waandishi wa habari, pia niaba yangu na Wasafi Classic, tungependa kuchua nafasi hii kuwashukuru watanzania wote pamoja na wanahabari, kwani siku zote mmekuwa mkinisaidia kunitangaza na kufikisha ujumbe kwa watanzania na najivunia nyinyi pia kwa kunifikisha hapa nilipo,”alisema.
“Mwisho mwa wiki hii nimetwaa tuzo ya MTV ikiwa ni tuzo yangu ya 11 ya kimataifa. Tuzo hii imenipa nguvu na ari mpya na dhamira yangu ni kufika kule ambako siku zote nimekuwa nikiota na kupamba ili kufikia mafanikio ya juu,” alisema Diamond.
Pia Diamond aliwataka wasanii kuungana kwa pamoja ili kuufikisha muziki wa bongo flava mbali zaidi na kuleta heshima kwa taifa.
“Ifike sasa, kila msanii wa hapa nyumbani kupigania kwa maarifa yetu yote kuhakikisha kazi zetu zinachomoza nje na kukubalika.
"Mimi sikupigiwa kura na watanzania pekee katika tuzo hii ya MTV wapo mashabiki wangu wengi wa nje wameniunga mkono, lakini hiyo inatokana na nguvu kubwa kutoka kwa watanzania ambako ndiyo chimbuko langu.
"Ni vyema sasa vita vyetu viwe vya kujiendeleza kusonga mbele nje ya mipaka ya nchi hii kama ilivyo wasanii wa Kimarekani ama Nigeria, nina imani ipo siku tutafika na tena ukaribu wake nauona na imani yangu si chini ya wasanii 10 watakuwa nyota nje ya mipaka ya Tanzania hivi karibuni,” alisisitiza.
Pia Diamond hakusita kuzungumzia wasanii wenzake waliotajwa kwenye tuzo za Afrimma pamoja na safari yake ya kuelekea Afrika Kusini kuwania tuzo ya African Achievement Award.
“Mwaka huu 2015 nimekuwa mmoja wa wanaowania tuzo za Afrimma ambazo nimeingia katika category 7 na pia nipo katika kinyang’anyiro cha tuzo za NEA America mwaka huu. Haya ni mafanikio.
"Pia kuwa wasanii wenzangu wametajwa kwenye tuzo za Afrimma, akina Alikiba, Mrisho Mpoto, Sheddy Clever, Vanessa na Ommy Dimpoz, hivi ndio vitu tulikuwa tunavitaka.”
Katika hatua nyingine Diamond alisema maneno ya mafumbo ambayo amekuwa akiyaandika kwenye mitandao ya kijamii anayaandika kuwachangamsha watu wake na sio kumlenga mtu.
“Unajua mimi nimekulia Tandale ni mswahili kabisa, na uswahili wangu ndio umefanya nikawa hapa. Tangia naanza Nenda Kamwambie ukisikiliza nyimbo zangu ni za Kiswahili, yaani mimi najiwekea kama ni furaha kwa kuwafurahisha watu.
Post a Comment