OBAMA AFUNGA ANGA LA KENYA KWA DAKIKA 50.
ZIARA ya kihistoria ya Rais wa Marekani, Barack Obama nchini Kenya inatarajiwa kusimamisha shughuli nchini kwa muda kupisha ujio wa kiongozi huyo wa taifa kubwa, lenye nguvu za kijeshi, kisiasa na kiuchumi duniani.
Miongoni mwa shughuli zitakazosimama ni usafirishaji wa anga, kwani mamlaka inayosimamia safari za ndege nchini Kenya (KCAA), imetangaza kuwa anga la Kenya leo litafungwa kwa dakika hamsini ili kuruhusu ndege ya Obama kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, jijini Nairobi. Kwa mujibu wa shirika hilo, agizo hilo litatekelezwa katika viwanja vyote vya ndege vya Kenya na kuwa anga hiyo itafunguliwa baada ya ndege hiyo ya Rais Obama itakapokuwa imetua.
Shirika hilo limeyaandikia mashirika yote ya ndege na pia kampuni zote za usafiri kuhusiana na agizo hilo na kuwa safari za ndege kadhaa zitacheleweshwa leo na Jumapili, ambapo zitachelewa kwa dakika 40 wakati Rais Obama atakapokuwa akiondoka Kenya kwenda Addis Ababa, Ethiopia.
Awali, Idara ya Polisi nchini Kenya ilikuwa imetangaza kuwa anga lote la Kenya lingefungwa siku tatu kabla ya ziara hiyo. Lakini, kwa mujibu wa KCAA ndege zote zinazopaa chini ya futi 20,000, hazitaruhusiwa kutua katika uwanja wa Jomo Kenyatta na ule wa Wilson mjini Nairobi leo hadi Jumatatu.
Agizo hilo sasa linamaanisha ndege zote ndogo, ambazo huhudumu kati ya Nairobi na Somalia na viwanja vingine vidogo katika kanda ya Afrika Mashariki, hazitaruhusiwa kutua Nairobi hadi mkutano wa kimataifa wa kibiashara ambao Obama atahudhuria utakapomalizika.
Obama anatarajiwa mjini Nairobi siku ya Ijumaa usiku, ambapo anatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kibiashara pamoja na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta. `Marufuku’ hiyo inagusa pia baadhi ya barabara muhimu za Jiji la Nairobi, ambazo zitafungwa kupisha ugeni mzito wa Obama ambaye anatua Kenya kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Marekani, licha ya ukweli kwamba ana asili ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Baba wa Rais Obama, Dk Hussein Obama ambaye kwa sasa ni marehemu, ni mwenyeji wa kijiji cha Kogelo ambako rais huyo wa Marekani, amewahi kutembelea kuona ndugu zake kwa upande wa baba.
Licha ya Ubalozi wa Marekani kutangaza kuwa Rais Barack Obama hakusudii kutembelea kijijini Kogelo, Magharibi mwa Kenya, bado matarajio ni makubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo. Kogelo, kijiji ambacho hakikujulikana hata nchini Kenya zaidi ya miaka kumi iliyopita, hivi sasa kinatajwa katika magazeti, redio na televisheni kote duniani, kama nyumbani kwa baba yake Rais Barack Obama, Barack Hussein Obama Senior.
Makaburi ya babu yake Rais Obama, Hussein Onyango Obama na Barack Obama Senior, yamewekwa vigae vipya na tayari kokoto zimemwagwa pembeni kuzuia vumbi iwapo wageni watakuja.
Aidha, makazi ya Mama Sarah Obama, bibi wa Rais Obama yamekuwa yakiboreshwa zaidi, huku wakazi wa kijiji hicho wakihoji sababu za kupuuzwa na serikali ya Marekani, wakidai Obama alistahili kwenda kusalimia ndugu zake.
Hata hivyo, Mama Sarah amedai kuwa alipokutana na Rais Obama Novemba mwaka jana huko Marekani, alimweleza angekuja kuzuru kaburi la baba yake. “Lazima atafika hapa kuona kaburi la baba yake,” alisema Mama Sarah Obama.HABARI LEO
Post a Comment