Header Ads

Mwigulu Nchemba ahojiwa Takukuru.


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Singida inamhoji Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kuhusiana na tuhuma za kukiuka Sheria ya gharama za Uchaguzi na Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini.
Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya wagombea ubunge watatu kati ya wanne wanaogombea jimbo la Iramba, mkoani hapa kugomea mchakato wa kampeni kuelekea kura za maoni wakidai baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa walikuwa wakimbeba mgombea mwenzao, Mwigulu Nchemba.
Wagombea waliogomea zoezi hilo ni Juma Killimbah, David Jairo na Amon Gyunda ambao walisema waliamua kuchukua hatua hiyo kutokana na msimamizi wa uchaguzi kura za maoni CCM katika jimbo hilo, Mathias Shidagisha na msaidizi wake, Mwita Raphael, kubariki wao kuchezewa rafu na Nchemba.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida Joshua Msuya alisema kuwa Nchemba anahojiwa kutokana na madai ya kukiuka makatazo mbalimbali yaliyoainishwa kwenye Sheria za Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema kuwa makatazo hayo yanajumuisha vitendo vyote vinavyokiuka sheria hiyo kabla ya kampeni, wakati wa kampeni na baada ya kampeni ambapo baada ya uchunguzi wa kutosha kukamilika jalada husika hupelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa uamuzi wa mwisho.
Kutokana na malalamiko mbalimbali kuifikia ofisi ya TAKUKURU, Msuya ametoa tahadhari kwa wagombea wote wa udiwani na ubunge mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vyovyote vinavyoashiria kushawishi wanachama kuwachagua vinginevyo wakigundulika hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.
Wakati kampeni zinaendelea kwenye majimbo mbalimbali mkoani hapa, vitendo vya ukiukwaji wa Sheria ya gharama za Uchaguzi vimekuwa vikiripotiwa kwa wingi kuliko wakati mwingine wowote wa kipindi cha uchaguzi.
Aidha, inaripotiwa kuwa hali si shwari katika jimbo la Mkalama kutokana na baadhi ya wagombea wenye uwezo kifedha kudaiwa kumwaga fedha na zawadi mbalimbali kwa wanachama na wananchi wa kawaida ili wagombea hao waweze kuwachagua siku ya kura za maoni itakapofika.HABARI LEO

No comments