Header Ads

MBEYA WAJIKATA BAADA YA LOWASSA KUKATWA.


Image result for LOWASSAImage result for LOWASSA
HATUA ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwaengua wanachama wake walioaminika kuteuliwa na chama hicho kukiwakilisha kwenye kinyang’anyiro cha urais baadaye mwaka huu, imeleta faraja mkoani Mbeya, ikiaminika kuwa hiyo ni hatua iliyondoa matumizi ya fedha katika uchaguzi.
Ni hatua inayoelezwa kumaliza takribani miongo miwili ya nguvu ya fedha kuchagua viongozi, kwa maana ya matumizi makubwa ya fedha katika Uchaguzi Mkuu.
Kuenguliwa kwa wanasiasa hao vigogo, walioelezwa kuwa na matumizi makubwa ya fedha katika mchakato wa kuomba kuteuliwa na chama chao katika nafasi hiyo ya urais, angalau kumerudisha matumaini ya kudhibitiwa kwa matumizi ya fedha kununua madaraka.
Faraja hiyo inatokana na imani iliyojengeka kwamba vigogo hao walitumia nguvu kubwa ya fedha kuitafuta nafasi hiyo, huku wakiandaa watu wao katika nafasi mbalimbali za uogozi, hususan, kwenye nafasi ya ubunge.
Wagombea waliotajwa zaidi kuwagawa wanachama wa chama hicho ni waziri mkuu aliyejiuzuru kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa, Bernad Membe.
Vigogo hao walitengeneza mitandao iliyodaiwa kutumia zaidi fedha kuwanadi watu wao, hatua iliyojenga hofu miongoni mwa wanachama wengine waliokuwa nje ya mitandao hiyo.
Zipo taarifa za baadhi ya wapambe kununuliwa vitendea kazi kama vile magari, kompyuta mpakato na simu kwa ajili tu ya kufanikisha kazi ya watu wao. Ni taarifa zilizotokana na tambo za wapambe hao mkoani humo, wakijiona kuwa tayari wamekamata dola.
Matarajio ya wapambe kutoka kwa wagombea urais
Yapo makundi mawili yaliyoumia kutokana na kuenguliwa kwa vigogo hao, la kwanza likiwa waliotarajia kuingia bungeni kwa ufadhili wao, baada ya kukatwa wamelazimika nao kujiengua kwenye kinyang’anyiro cha ubunge.
Pamoja na kuingia kwa vishindo majimboni wakidai wameshawishiwa na wazee, watangaza nia hao hawakuonekana kuchukua fomu wala kurudisha.
Katibu Msaidizi, CCM Mbeya Mjini, Neema Lunda amethibitisha kuhusu mmoja wa watangaza nia katika jimbo hilo, Thom Mwang’onda kutochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ya ubunge, Jimbo la Mbeya Mjini.
“Wapo watu wameathrika na hatua ya CCM kuengua watangaza nia ya urais, lakini ni advantage kwa vyama vya upinzani mkoani Mbeya, sasa nguvu ya pesa haitakuwapo, matumizi ya pesa yanaingiza watu wasiokuwa na sifa,” anasema Godfrey Mwandulusya.
Kwa mujibu wa Mwandulusya, baadhi ya watu walionyesha nia ya kugombea ubunge kwenye jimbo hilo, walifanya hivyo wakitarajia kubebwa na fedha za watu wao, kwamba walikuwa kwenye hizo kambi kimaslahi zaidi.
Kundi la pili lililoumizwa na hatua hiyo ya CCM kuwatosa vigogo wake ni la wasaka vyeo, wapo waliojitangaza kushika nafasi za ukuu wa wilaya na mkoa, kundi hili linabeba wapiga debe wengi wa kutoka mkoani Mbeya.
Wapo pia waliotarajia uwaziri, miongoni mwao ni waliokimbilia kwenye nafasi za ubunge, wakiamini kwamba watapita kutokana na nguvu ya fedha ya mtu wao na hatimaye kuteuliwa kwenye nafasi hiyo.
“Usione watu wanaweweseka, watu walishajipanga kwenye nafasi ya waziri mkuu, waziri wa fedha, ujenzi na uchukuzi,” anasema mmoja wa wabunge waandamizi kutoka mkoani Mbeya, akiomba kutotajwa jina.
Watu walilazimishwa kulisikiliza jina la mtu wao na uwezo wake kifedha na kiuongozi. Kwenye maeneo ya starehe, hususan, ulevi, saluni, vijiwe mbalimbali mjini, watu walilazimishwa kusikiliza na kumjadili mtu wao, wakisukumwa na nguvu ya maslahi binafsi.
Miongoni mwa maeneo yaliyopata shida mwaka huu ni pamoja na Jimbo la Kyela, ambako hali ilikuwa mbaya zaidi, japo sasa pametulia, watu wamerudi kwenye akili zao, busara zimerudi tena, na wameanza kuheshimiana tena.
Kubadilika ghafla kwa upepo wa kisiasa mkoani humo, kumethibitika wilayani Kyela mwisho mwa juma lililopita kwa kundi kubwa la wakazi wa wilaya hiyo, wakiongozwa na wazee, kuamua kumchukulia fomu mbunge wao, wakibainisha kuwa hawako tayari kutishwa na watu wenye dhamira ya kuwachagulia viongozi.
Wananchi hao waliamua kuchanga fedha za kuchukulia fomu ambapo zilipatikana shilingi 1, 002,000 hivyo kufanikisha zoezi hilo. Katika maelezo kuhusu uamuzi wao huo, wananchi hao wanasema wameamua kumchukulia fomu baada ya mbunge huyo kutoonekana wilayani humo, walihofu angechelewa, hivyo ingekuwa hasara kwa wilaya kwani waliopo wanawaona hawatoshi.
Utulivu wa kisiasa umeweza kuonekana wilayani Kyela, Rungwe, Mbeya Mjini, na maeneo mengine ya mkoa huo ambako tangu mwanzoni mwa mwaka huu kulivurugwa na siasa za uchaguzi, hususani nafasi ya urais.
“Vurugu hakuna, kumetulia, watu wame appreciate, hali ni shwari kwa kweli,” anasema Katibu CCM Wilaya ya Kyela, Eva Degeleki, katika mahojiano yake ya simu na Raia Mwema.
Zipo taarifa kwamba vurugu za kisiasa mkoani Mbeya zimekuwa zikifadhiliwa na wanasiasa kutoka nje ya Mkoa huo, wanasiasa ambao waliojiandaa kukamata dola katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.
Katika kitabu chake “Sauti ya umma ni sauti ya Mungu, Prof Mark Mwandosya analibainisha hilo anapoelezea jinsi “wakubwa” walivyofadhili anguko lake katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), lakini mwisho wa yote wakashindwa baada ya wananchi kusema hapana, naye akaibuka mshindi.
Ni uchaguzi unaobaki katika historia ya Mkoa huo, watu walishuhudia matumizi makubwa ya fedha na nguvu ya dola kuhakikisha Profesa Mwandosya anaanguka. Hata hivyo, mwisho wa yote alishinda na ndipo akawiwa kuandika kitabu hicho kama somo kwa wasaka madaraka kwa kutumia nguvu za fedha na dola, wakipuuza nguvu ya umma.
Wagombea waanza kujinadi Mbeya;
Pilika pilika za kujinadi kwa wanachama kwa waombaji wanafasi ya ubunge mkoani Mbeya zimeanza Jumatatu ya juma hili, ambapo wagombea hao watazungukia kata zote katika majimbo yao kabla ya kufanyika uchaguzi wa uteuzi wa wagombea kwa kila jimbo.
Kwa mujibu wa makatibu wa CCm Wilaya, idadi ya wanachama waliojitokeza kuwania nafasi ya ubunge kwa baadhi ya majimbo mkoani humo, idadi katika mabano, Busekole (12), Rungwe (7), Kyela (10), Lupa (7), Songwe (4), Mbeya Mjini (16) na Ileje (6).
Katika uchaguziwa mwaka huu, Chama cha Mapinduzi kinatarajiwa kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vyamavya upinzani, hususani CHADEMA, chama ambacho kimejitokeza kuwa mshindani mkubwa wa CCM mkoani humo.
Hata hivyo, kila chama kitalazimika kuwa makini katika uteuzi wa wagombea wake kutokana na wapiga kura wa Mkoa huo kuzingatia zaidi sifa za mgombea kuliko itikadi za vyama.

No comments