Header Ads

MAGUFULI:SITAOGOPA,SITAMWONEA YEYOTE.

Mgombea mteule wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli.(Picha na Yusuf Badi)

MGOMBEA mteule wa urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Dk John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan jana walipokelewa na umati mkubwa wa wakazi wa Dar es Salaam, bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Kutokana na mapokezi ya aina yake, Magufuli akitambulishwa kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam tangu alipopitishwa na chama chake kuwa mgombea wa urais mwishoni mwa wiki, aliendelea kusisitiza kuwalipa fadhila Watanzania kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuwaletea maendeleo.
Alisisitiza kuwa, katika utendaji wake kazi, kamwe hatawavumilia watendaji wazembe wasioisaidia serikali, huku akiapa kufanya kila linalowezekana kuondoa kero ndogondogo zinazowakabili wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga, wakiwemo mamalishe na waendesha bodaboda.
Dk Magufuli ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi, aliyasema hayo akiwa kwenye Viwanja vya Zakheem, Mbagala katika Manispaa ya Temeke.
Akizungumza katika viwanja hivyo, alisema iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi atahakikisha haki inatendeka kwa Watanzania wote.
“Nataka niseme kwa dhati sitawaangusha, nitafanya kazi kweli kweli, sitamuogopa mtu na wala sitapenda mtu wa chini aonewe,” alisema Dk Magufuli.
Aliongeza kuwa atahakikisha anasimamia Ilani ya CCM na kuitekeleza. Magufuli aliwashukuru Watanzania kwa sala zao kwani katika mchakato mzima alikuwa akiwasihi wamuombee.
“Kupitishwa kwangu inadhihirisha wazi mlikuwa mnaniombea na sala zenu zimesikilizwa na mwenyezi Mungu,” alisema.
Wazembe serikalini
Aidha, Magufuli amesema anachukizwa na watendaji wa serikali wasiowajibika, na kuahidi kuwashughulikia.
Magufuli ambaye alifika uwanjani hapo akisindikizwa na msafara mrefu wa magari ya wafuasi wake na kulakiwa na mamia ya wanachama na wasio wanachama alikuwa amefuatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida.
Pia walikuwepo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara, wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Dodoma, wakuu wa wilaya zote tatu, wabunge wa kuchaguliwa na kuteuliwa wa mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, Magufuli alisema anachukizwa na watendaji wa serikali wasiowajibika na kuhakikishia Watanzania kuwa atawaletea mendeleo bila kujali itikadi za vyama.
“Naomba mshikamano, kwani wanachohitaji Watanzania ni haki, maendeleo na kuondolewa kero zao na wamechoka kulalamika. Mimi sio mkali, mimi ni mpole ila ninawachukia watendaji wa serikali ambao hawatimizi wajibu wao, na hao nitalala nao mbele, ili Watanzania wa hali ya chini waweze kufaidi nchi, uhuru na maendeleo bila kuangalia itikadi ya vyama,” alisema.
Magufuli alisema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi, atafanya kazi bila kumwogopa mtu na wala hatataka mtu wa chini aonewe.
“Nitafanya kazi kweli kweli nikipewa ridhaa ya kuongeza nchi, sitamuogopa mtu na wala sitapenda mtu wa chini aonewe, kwasababu maonevu yamekuwapo."
Aidha, Magufuli aliahidi kusimamia vizuri serikali ili kuhakikisha kero ndogondogo zinafutika na kutekeleza ilani ya CCM ambayo imejumuisha mambo mengi na imelenga kushughulikia kero za wananchi.
“Ilani ya CCM imezungumza masuala mengi ya kilimo na biashara. Nitawalinda wafanyabiashara wadogo na wakubwa ili kusudi Watanzania wengi wapate ajira za kutosha. Tutasimamia yote. Sitafafanua yote.., jukumu letu ni kuleta maendeleo kwa watu wote, na maendeleo hayana chama ila ukweli ni kuwa maendeleo yanaletwa na kiongozi kutoka CCM."
Pia Magufuli alisema atahakikisha anaendeleza yote yaliyofanywa na viongozi wa awamu ya nne, na kumalizia yaliyoachwa kwa haraka. Alisema, pia uongozi wake utahakikisha unalinda misingi ya Watanzania na taifa, kwa kudumisha na kulinda amani na umoja wa Watanzania.HABARI LEO

No comments