Header Ads

MAGUFULI:NILIPANGA KUSTAAFU SIASA 2015.

MGOMBEA urais mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema kama si kuombwa kuwania urais, alipanga kuachana na siasa mwaka huu, kwani alijiwekea lengo la kuachana na ubunge baada ya kuwa mbunge wa Chato kwa miaka 20 sasa.
Alisema hayo mbele ya umati wa wakazi wa mkoani Geita na baadaye Jimbo la Chato waliojitokeza kumlaki, huku yeye mwenyewe akisema anaamini kwa aina ya mapokezi anayoyapata kila anakopita, ana imani CCM itavigaragaza vibaya vyama vya upinzani.
Magufuli aliyekuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1995,alisema alitarajia baada ya miaka 20 ya ubunge wake astaafu, kwani hakutaka tena kuendelea na shughuli za siasa, lakini baada kila kona ya nchi kuombwa kugombea, alichukua fomu kimya kimya na kuirudisha kimya, hivyo kuteuliwa kugombea urais ni matokeo ya maombi ya Watanzania.
Katika mkutano huo uliofanyika Stendi ya zamani ya Chato, mamia ya wananchi wa vyama mbalimbali vya upinzani, hususan Chadema walirudisha kadi zao na kujiunga na CCM.
Magufuli alisema maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mikoa aliyokwenda kujitambulisha ni salamu kwa wapinzani. “Nilitamani kikombe hiki kiniepuke, maana nilitaka baada ya miaka 20 ya ubunge nipumzike mwaka huu, lakini hili la urais limekuja baada ya kila kona ninayopita naambiwa kagombee urais, sasa nikaona ngoja nijaribu lakini sikulitilia maanani, ndio maana niliamua kufanya kimya kimya kila kitu, kwa bahati nzuri kikombe hiki kimekuja chenyewe, msiniangushe,” alisema.

Dk. Magufuli alisema atakuwa mwadilifu na katika utumishi wake na alitumia fursa hiyo kuwaaga rasmi wananchi wa jimbo lake, kwani hatagombea ubunge.

No comments