WAZEE NA WAGANGA WA TIBA ZA ASILI WALITAKA JESHI LA POLISI KUHESHIMU MILA NA DESTURI,TABORA.
Kufuatia zoezi la askari polisi kuwasaka waganga wa jadi wanaodaiwa kujihusisha na ramli chonganishi, waganga wa tiba za asili na wazee wa kimila wa jamii wa waswezi mkoani Tabora wamelitaka jeshi la polisi kutokamata vifaa vinavyotumika kwa masuala ya matambiko na kuvihusisha na matukio ya mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi albino kwani kufanya hivyo watakuwa hawatendi haki kwa jamii inayojali na kutekeleza mila na desturi za asili.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya Wafanyabiashara wa dawa na vifaa vya matambiko ya asili wa soko kuu la mjini Tabora wamelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana nao wakati wa kuendesha zoezi hilo badala ya kulifanya wao kama polisi kwakuwa wanadaiwa kukamata vitu ambavyo havihusiki na matukio ya mauaji na ramli chonganishi.
Baadhi ya wazee wa kimila akiwemo Mtemi wa Wayege na Wasyepe mkoani Tabora Habib Shaban Mrutu amesema wao kama wazee wanaotekeleza mila na desturi katika maisha yao hawapingi zoezi la kuwasaka watu wanaojihusisha na mauaji ya walemavu wa ngozi Albino bali kuna haja ya kuliangalia kwa kina zoezi hilo ili lisije likaathiri mila na desturi zao.
Akizungumza wakati wa hafla ya Matambiko ya Jamii ya Waswezi mjini Tabora, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora mjini Bw.Moshi Nkonkota amewataka Waganga wa tiba za asili na wazee wa kimila kulisaidia jeshi la Polisi kuwafichua waganga wasio waaminifu wanaopiga ramli chonganishi zinazodaiwa kuwa chanzo kikubwa cha mauaji mbalimbali yakiwemo yale yanayotokana na visasi.
Aidha katika hafla hiyo ya Matambiko ambayo hufanyika mara chache kulingana na matukio,Waswezi walimtambikia mlezi wao Bw.Emmanuel Mwakasaka aliyeshika wadhifa huo akiwa ni mtu wa pili baada ya kufariki Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa mlezi wa kwanza wa jamii ya Waswezi ambao asili yao ni mkoa wa Tabora.
Post a Comment