Header Ads

WAUZA MAFUTA WAPEWA ONYO.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage
SERIKALI imesema itawachukulia hatua kali wafanyabiashara wa mafuta, ikiwamo kuwafungia vituo vyao na pia kufuta leseni zao watakaobainika kugoma kuuza nishati hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage amewaonya wamiliki wa vituo vya mafuta nchini wasije wakajiingiza katika mtego wa kufanya mgomo wa kuuza mafuta katika vituo vyao.
Mwijage alitoa tamko hilo wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo Naibu Spika, Job Ndugai alimtaka atoe tamko la Serikali kutokana na taarifa zilizokuwa zikisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba wauza mafuta wamepanga kugoma kuuza mafuta kuanzia leo ili kusubiri bei mpya ya bidhaa hiyo.
Mwijage alisema naye ameona taarifa hizo kwamba ndani ya siku mbili zijazo kutakuwa na tatizo hilo la mafuta, lakini alilihakikishia Bunge kwamba kuna hifadhi ya kutosha ya nishati hiyo na hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu.
“Nimeona katika mitandao ya kijamii kwamba Taifa katika siku mbili zijazo litakuwa na uhaba wa mafuta. Niseme hili haliwezi kutokea. “Haliwezi kutokea na haya si maneno ya kufurahisha. Haliwezi kutokea kwa sababu tunajua kwa takwimu kwamba katika hifadhi za Dar es Salaam kuna mafuta ya kutosha. Tunajua hilo. “Haliwezi kutokea kwa sababu sheria na kanuni zinampa mamlaka Waziri kuruhusu mafuta yauzwe. Haiwezi kutokea kwa sababu sheria za Ewura zinaweza kufungia mtu yeyote mwenye mafuta anayezuia mafuta kuuzwa,” alisema Naibu Waziri huyo.
Alisisitiza kwa kuwaonya wenye mafuta nchini wasijiingize katika mtego huo kwa kutaka kufanya uvumi huo utokee na kuwa kweli kwani hakuna sababu ya kuzuia mafuta yasiuzwe.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Boniface Simbachawene pamoja na watendaji wengine wa wizara hiyo wanafuatilia jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kutafuta chanzo cha ujumbe huo.
Aliwataka wenye mafuta kuruhusu yauzwe na watakaoenda kinyume basi vituo vyao vinaweza kufungiwa na wale wenye hifadhi ya mafuta pia vitafungiwa na leseni itachukuliwa kwa vile hiyo ni mali ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya nishati na madini.
Juzi mitandao mbalimbali ya jamii nchini ilikuwa na habari za kuwataka wananchi kuweka mafuta kwa wingi kwenye magari yao kwa vile wenye mafuta walikuwa wamepanga kugoma kuyauza kwa siku mbili zijazo, lengo ikiwa ni kusubiri bei mpya kutoka Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Gesi (Ewura).
Pamoja na agizo hilo la Serikali, gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam, jana vilishindwa kutoa huduma kutokana na kuwepo kwa madai ya wauzaji wa jumla kugoma kuuza bidhaa hiyo wakisubiri kupanda kwa bei ili waweze kuuza kwa bei mpya.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vituo vikiwa havitoa huduma kabisa huku baadhi vikitumia pampu moja kutoa huduma hiyo jambo lilisababisha foleni na kadhia kwa wateja waliokuwa wakihitaji huduma hiyo.
Hata hivyo, vilikuwepo baadhi ya vituo vilivyoendelea kutoa huduma hiyo kama kawaida, ikiwemo vilivyopo katikati ya jiji. Vituo zaidi ya sita katika maeneo mbalimbali ya jiji hili vilikuwa havitoi huduma huku vingine vikitoa kwa kutumia pampu moja pekee.
Katika eneo la Keko kulikuwa na shida ya nishati hiyo, ambapo mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha mafuta kilichopo eneo hilo alidai kuwa hawana mafuta na hawajui ni muda gani wataweza kupata nishati hiyo ili waendelee kutoa huduma.
Aidha, katika eneo la Tabata hali ilikuwa ni mbaya zaidi hasa kuanzia kwenye vituo vya kuuzia mafuta vilivyopo eneo la Tabata Muslim kushindwa kutoa huduma kwa kisingizio kuwa yalikuwa yamekwisha.
Katika kituo cha Tabata Relini, hali ilikuwa pia mbaya kwa kuwa kulikuwa na sehemu moja tu iliyokuwa ikiuza mafuta hayo na penyewe walikuwa wakisubiria yaishe na wafunge.
Juzi kulikuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwa kutakuwa na shida ya huduma hiyo kutokana na wauzaji wa jumla wa mafuta kugoma kuuza wakisubiria kupanda kwa bei. Kwa upande wake Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura) imekanusha taarifa za kuwepo kwa uhaba wa mafuta nchini.
Akizungumza na wandishi wa habari, Ofisa Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alisema kuhusu suala la wauzaji wa kubwa kufungia mafuta ili kusubiri bei ipande hana uhakika nalo hivyo lazima wafanye uchunguzi ili kubaini kama ni kweli.
“Siwezi kusema kweli au si kweli lazima tufanye uchunguzi ili tubaini kama kuna ukweli kuhusu taarifa hizi na jana tumepita katika sehemu mbalimbali kufanya uchunguzi,” aliongeza Kaguo.HABARI LEO.

No comments