TALK SHOW ZA BONGO NA CHANGAMOTO ZAKE.
MIONGONI mwa vipindi vya televisheni maarufu duniani ni vile vya Oprah Winfrey Show cha Oprah Winfrey na The Tyra Banks Show cha Tyra Banks.
Hivi vyote vinaendeshwa na watangazaji wanawake ambao ni Wamarekani wenye asili ya Afrika. Kwa ujumla wamefanikiwa kujizolea umaarufu duniani kote kwa umahiri wao.
Kazi yao kwa namna nyingine imeibua watangazaji wengi wa aina hiyo katika mataifa mengine ambao nao wanazo ‘Talk Show’ zao zinazofanya vizuri.
Kazi yao kwa namna nyingine imeibua watangazaji wengi wa aina hiyo katika mataifa mengine ambao nao wanazo ‘Talk Show’ zao zinazofanya vizuri.
Kwa Tanzania tayari sasa ina vipindi vinne vya aina hiyo ambavyo ni The Sporah Show cha Irene Sporah Njau, The Mboni Show cha Mboni Masimba, Ongea na Janet cha Janet Sosthenes Mwenda na Wanawake Live cha Joyce Kiria.
Kwa mwenendo wa vipindi hivi, bila shaka baada ya mwaka mmoja, huenda kukaibuka vipindi vingi zaidi kutokana na mwelekeo wake wa kukubalika.
Lakini wakati vipindi hivyo vikiibuka pia kuna swali linakuja, nalo ni je, Watanzania wanafuata misingi na kanuni za uendeshaji wa vipindi hivyo?
Hellen Humphrey, mkazi wa Dar es Salaam anasema: “Huwa ninapata shida kuwaelewa watangazaji wa hizi Talk Show zetu, wengi huanza vizuri, lakini baadaye wanaboronga, wanatoka nje ya mada.”
Kiria (31) wa Wanawake Live kinachoonyeshwa na EATV, anakiri bado kuna safari ndefu kufikia kiwango cha Oprah, lakini anaamini wako katika mwenendo sahihi.
“Unajua huwezi kulala na kuamka na ukawa kama Oprah, hata vitendea kazi vyetu bado viko chini,” anasema Kiria mmiliki wa Local Media Entertainment yenye hakimiliki ya kipindi hicho.
Irene Sporah kwa upande wake anasema: “Changamoto zipo, kubwa na watazamaji kutufananisha na akina Oprah, wenzetu wametutangulia. Pia kuna masuala ya lugha, lakini naamini tunao uwezo mkubwa.”
Mtangazaji huyo ametokea katika biashara ya nguo na vitu vingine vya urembo wa wanawake.
Mboni Masimba aliyewehi kushiriki mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, yeye anasema pamoja na wanawake kufanya mengi mazuri, lakini bado kuna changamoto wanazokumbana nazo.
“Lakini kwa upande wangu ninajitahidi kuondoa dhana ya kuwa hatuwezi, kipindi changu kitakua uthibitisho wa kuelezea nafasi ya mwanamke katika jamii,” anasema.
Naye Janet Mwenda anasema changamoto ni nyingi hasa wakati wa utayarishaji wa vipindi hivyo kutokana na ukosefu wa wadhamini.
“Kazi tunaiweza, ndiyo maana tunaifanya. Ila suala la ukosefu wa wadhamini linafanya vipindi vingi vya Talk Show hapa Tanzania kukosa ubora unaotakiwa,” anasema.
Post a Comment