Header Ads

KINGUNGE ANUSA MCHEZO MCHAFU URAIS NDANI YA CCM.


Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru. 

 Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru (Pichani) amesema anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza kuwa ni ishara mbaya.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais wa awamu zote nne, pia, bila kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kujibu kauli ya makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliyekaririwa akisema kuwa mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.
Kingunge, ambaye amejitokeza hadharani kumpigia debe Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka wadhamini mkoani Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani Kinondoni.
Hadi sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM ni 41 baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana akisema atamudu kupata wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano zilizosalia. Akizungumza katika mkutano wa kusaka wadhamini ulioandaliwa kwa ajili ya Lowassa wilayani Kinondoni jana, Kingunge alipingana na kauli ya Mangula kuwa mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi mwenyewe akisema chama hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na nje.
Siku tatu zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa anatakiwa kunadiwa na chama.
Lakini Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema chama hicho kimeweka utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza kuwahukumu wagombea kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi kuwahukumu wagombea kabla katika chaguzi zilizopita.
“Mchakato ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema Kingunge ambaye aliibuka Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli zake jijini Dar es Salaam.
“Nimemsikia kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi hapa, nikamuona kwenye televisheni anasema mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi, ananadiwa na chama.
“Nikasema eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze yeye na wenye fikra kama hizo kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu wetu; kwanza, mwanachama anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima ajinadi ndani ya chama, ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa katiba na taratibu zetu. Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”
Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.
“Si vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama wakaanza ama wakaendelea kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi. Kama wana mashaka tupo tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku akishangiliwa na mamia ya watu.
Kingunge alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa Dodoma alisema chama kinatafuta mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho ili kuweza kushindana na vyama vingine.

No comments