KINANA AITOLEA UVIVU SERIKALI YA CCM.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameikosoa Serikali ya chama chake kwamba imekuwa siyo sikivu kwa matatizo ya wananchi na kuwa wabunge wa chama hicho wanapitisha sheria ambazo zinakuwa mzigo kwa wananchi.
Akihutubia katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake, jijini Mwanza jana, Kinana alisema atafanya kikao cha kwanza na wabunge wa CCM baada ya uchaguzi ili kuwaeleza majukumu yao ya msingi ikiwamo kuiwajibisha Serikali.
Alisema wabunge wa CCM wamekuwa wakiunga mkono kila jambo linaloletwa bungeni bila kutathmini matokeo ya sheria hizo kwa wananchi wanaowawakilisha.
Alisema lazima ifike wakati wabunge wa CCM wabadilike na kuwatumikia wananchi wao.
“Nitakutana na wabunge wa CCM na kuwaambia kwamba sheria walizozipitisha haziwasaidii wananchi… lazima chama kiwe na nguvu ya kuielekeza au kuiwajibisha Serikali yake,” alisema Kinana huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Katibu Mkuu huyo alisema kuna haja ya kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wa chama na mojawapo ni kuchagua mtu mwingine wa kuongoza wabunge wa CCM bungeni badala ya Waziri Mkuu kama ilivyo sasa.
Alisema Waziri Mkuu ataachwa atekeleze jukumu lake la kuiongoza Serikali bungeni, lakini kuwe pia na kiongozi wa wabunge wa CCM bungeni. Alisema mfumo huo utakipa chama nguvu zaidi ya kuisimamia Serikali yake.
“Wamekaa wabunge tena na kupitisha sheria ya kila gari kuwa na kizimamoto, nani alisema gari langu lina mpango wa kuungua?” alihoji kiongozi huku na kusema sheria nyingine zinatakiwa kufutwa kwa sababu hazimsaidii mwananchi.
Aliishangaa Serikali ya CCM kwa kushindwa kufuta baadhi ya sheria ambazo zimebainika kuleta usumbufu kwa wananchi na kusisitiza kuwa lazima ifike wakati Serikali ifanye tathmini ya sheria zake na kuzifuta ambazo hazifai kwa sasa.
“Nimekuwa waziri na kiongozi serikalini kwa muda mrefu, lakini sijawahi kuona Serikali ikifuta sheria. Wamekuwa wakiongeza sheria mpya kila siku. Hivi karibuni Serikali imepeleka miswada mingine 11 na yote imepitishwa. Kwa namna hiyo tunambebesha mwananchi mzigo mkubwa,” alisema.
Kinana aliitaka Serikali kuwashirikisha wananchi wakati wa kutunga sheria ili kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Post a Comment