Header Ads

KENYA KUTOLEGEZA KAMBA KATIKA KUPAMBANA NA UGAIDI.

Kenya kutolegeza kamba katika kupambana na ugaidi


Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa, kuna udharura wa kuchukuliwa hatua zaidi za kupambana na ugaidi. Rais Kenyatta amesema kuwa, nchi yake inashirikiano na asasi za kiraia, sekta binafsi, nchi jirani pamoja na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kupambana na kukabiliana na ugaidi. Rais wa Kenya amesisitiza kuwa, hakuna nchi ambayo imesalimika na tishio la ugaidi, hivyo kuna haja ya kuweko ushirikiano ili kung’oa mizizi ya ugaidi. Akihutubia kongamano la kieneo kwa ajili ya kujadili ongezeko la makundi yenye kufurutu ada mjini Nairobi, Rais Kenya amesema bayana kwamba, Kenya katu haitasalimu amri mbele ya makundi ya kigaidi na kwamba, itaendeleza vita vyake dhidi ya ugaidi. Kuhusiana na wanamgambo wa al-Shabab ambao wamekuwa wakiishambulia Kenya mara kwa mara, Rais Kenytata amesema kuwa, kundi la al-Shabab limeishiwa nguvu na kwamba mashambulio yake ni ya kulinusuru tu kundi hilo, na si ya kutafuta ushindi. Kongamano la kieneo kwa ajili ya kujadili ongezeko la haraka la makundi yenye kufurutu ada katika nchi za Afrika lilianza siku ya Alkhamisi mjini Nairobi. Wawakilishi wa serikali za Kiafrika, wanasiasa na wataalamu kutoka karibu nchi 40 walishiriki katika kongamano hilo la lililotazamiwa kuhitimisha shughuli zake jioni ya jana Jumamosi.

No comments