Header Ads

JK:WAUZA UNGA HAWATANYONGWA.


Rais Jakaya Kikwete akizindua huduma ya simu ya 117 itakayosaidia kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya dawa za kulevya. Kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya vijana Tanzania (Tayoa) Peter Masika na kushoto ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid 


Bagamoyo. Rais Jakaya Kikwete amesema amesaini sheria mpya ya dawa za kulevya ya mwaka 2015, itakayoanza kutumika kabla ya Oktoba na wauzaji wake hawatanyongwa bali watafungwa maisha.
Akizungumza jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya na Usafirishaji Haramu, Rais Kikwete alisema sheria hiyo itazaa taasisi maalumu ya kushughulikia mianya yote inayotumiwa na wafanyabiashara wa ndani na nje.
“Sheria hii mpya nina hakika kabisa itasaidia kutokomeza mianya ya uingizwaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya nchini,” alisema Rais Kikwete.
Alisema sheria hiyo itazaa taasisi hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuwakamata na kuwashtaki wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo, huku ikishirikiana na DPP na mhusika akikamatwa atafungwa kifungo cha maisha jela.
Alisema anaondoka madarakani huku sheria hiyo ikiwa tayari imeanza kufanya kazi na atahakikisha inapitishwa mapema ili Rais ajaye akute taasisi hiyo imeanza kazi.
“Sheria hii ambayo tayari nimeshaweka saini ina majibu yote ya Watanzania waliyokuwa wakijiuliza kwa miaka yote kuhusu mianya inayotumika kuingiza dawa hizi haramu nchini. Pia, ni sheria itakayotupatia ufumbuzi wa matatizo ya sasa na miaka ijayo itazaa taasisi itakayoratibu, pambana, kamata, peleleza na hata kupekua ikibidi ili kutokomoza janga hili,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ili kupambana na hali hiyo, Serikali imeimarisha vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya sambamba na tume ya kudhibiti na kupambana na dawa hizo, polisi ambao wamepewe mamlaka ya kukamata wafanyabiashara na watumiaji wa dawa hizo.
“China wananyonga, lakini hapa kwetu tutawafunga maisha, wafanyabiashara hawa wamekuwa wakiwatumia watu maarufu, wasanii, waigizaji na hata wachezaji mpira kote duniani ili kuhakikisha kwamba wanajipatia fedha nyingi,” alisema.
Aliongeza: “Lazima Watanzania tuhakikishe tunatokomeza kwa kushirikiana na kikosi kazi ikiwamo tume na polisi ili kuhakikisha tunafichua mianya hii kwa ajili ya kulinda vizazi vyetu maana athari zake ni kubwa.”
Hata hivyo, JK alipiga vita matumizi ya shisha akisema kuwa yana madhara makubwa kwa afya ya binadamu.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UN), Philippe Poinsot alisema, ingawa jamii ya kimataifa inaongeza juhudu endelevu bado tatizo la dawa za kulevya duniani ni tishio kwa afya ya jamii, ulinzi na usalama wa maisha ya vijana wadogo, usalama wa kimataifa na mipaka yake na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na utulivu.
“Hali hii imesababisha Tume na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya (UNODC), kuendelea kufanya kazi yake ya kimataifa kudhibiti hali hiyo na kuziomba Serikali duniani kujitolea kwa hali ya juu, kifedha na kisiasa kuunga mkono shirika hilo,” alisema Poinsot.MWANANCHI

No comments