IDADI ya wana CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho ili kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, leo itaongezeka na kufikia wagombea 40.
Hali hiyo inatokana na mwana CCM, Helen Elinenga, anatarajiwa kuchukua fomu katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma.
Idadi ya wagombea waliorudisha fomu wamefikia wanane ambapo jana waliorudisha fomu ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mathias Chikawe, mwanachama wa CCM, Bw. Boniface Ndengo na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Titus Kamani.
Baada ya kurudisha fomu hizo, Bw. Chikawe hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari kama ilivyo kwa wagombea wengine waliorudisha fomu hizo.
Kwa upande wake, Bw. Ndengo alisema amekutana na changamoto kubwa alipozunguka zaidi ya mikoa 20 ikiwemo mitatu ya Zanzibar kwani baadhi ya wana CCM walikataa kumdhamini wakitaka fedha ambazo hakuwanazo kama walivyofanya wagombea wengine.
"Kuna wagombea wanatumia fedha nyingi ili kuhakikisha wanapata uongozi jambo ambalo halifai kufumbiwa macho, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mtu anayetumia rushwa kusaka uongozi anatakiwa kuogopwa kama ugonjwa wa ukoma.
"Nimeshuhudia mwenyewe wananchi wa kawaida nao ni zao la rushwa kwani baadhi ya sehemu nilikataliwa kudhaminiwa kwa kuwa sikutoa fedha kama walivyofanya wenzangu ambao siwezi kuwataja majina," alisema.
Naye Dkt. Kamani alisema wadhamini wake wote wanatoka katika kata na tarafa zilizopo vijijini kwani asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi huko ndio maana aliamua kuwa na wadhamini hao.
Alisema amefika mikoa 17 ikiwemo mitatu ya Zanzibar na 12 ya Tanzania Bara na amepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wana CCM kwenye maeneo yote aliyopita.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo leo anatarajiwa kurudisha fomu yake akiwemo na Leonce Mulenda baada ya kukamilisha taratibu za kutafuta wadhamini.
Post a Comment