Header Ads

HUKUMU YA MRAMBA NA WENZAKE LEO.

Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba
HUKUMU ya kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 inayowakabili Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja inatarajiwa kutolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jopo la mahakimu watatu, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela, linatarajia kutoa hukumu hiyo baada ya kupitia ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Upande wa Jamhuri uliita mashahidi saba na mahakama iliwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu, na katika utetezi wao washitakiwa walijitetea wenyewe na kuita mashahidi wawili. Baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao, mahakama imetoa nafasi kwa pande zote mbili kuwasilisha hoja za kuishawishi kuwaona washitakiwa hao wana hatia au hawana hatia.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008 ikiwa ni miaka sita iliyopita, wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Katika utetezi wake, Mramba alikiri kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa kuwa kulikuwa na mkataba uliosainiwa Juni 2003 kati ya kampuni hiyo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao ulikuwa unaonesha malipo yafanyike bila ya kukatwa kodi.
Mgonja alidai kuwa yeye ndiye aliyemshauri Mramba kuisamehe kodi kampuni hiyo kutokana na mkataba huo. Hata hivyo, inadaiwa msamaha wa kodi ulitolewa wakati tayari Wizara ilikuwa imepokea barua za kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zilikuwa zinakataza kampuni hiyo isisamehewe kodi.
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa Sh mlioni 207 kutoka katika akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayomkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na wenzake wanne kwa kuwa mshitakiwa mmoja amelazwa.
Jopo la Mahakimu watatu linaloongozwa na Hakimu Mkazi, John Utamwa, Ignas Kitusi na Eva Nkya liliahirisha hukumu hiyo hadi Julai Mosi mwaka huu baada ya kuelezwa kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Madeni ya Nje ( EPA), Iman Mwakosya amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Watu wenye matatizo ya akili.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, mahakama imesema itaandika barua kupeleka katika Hospitali Muhimbili, wafahamu hali ya kiakili aliyonayo Mwakosya kama ataweza kuelewa mwenendo wa mahakama , ili waweze kusoma hukumu hiyo.
Mbali na Maranda na Mwakosya washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Farijala Hussein ambaye anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa EPA, Ester Komu na aliyekuwa Katibu wa BoT, Bosco Kimela.
Wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh milioni 207 kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Washitakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo, kughushi na kuiba zaidi ya Sh milioni 207 kutoka BoT, aidha wanadaiwa kughushi nyaraka ikiwamo hati ya makubaliano ya kuhamisha deni kutoka kampuni ya General Marketing ya India kwenda kampuni ya Rashaz (T) ya Tanzania na kuiba fedha hizo .HABARI LEO.

No comments