HARUSI YA OKWI YAFUNIKA UGANDA.
Mshambuliaji wa Simba ,Emmanuel Okwi akiwa na mkewe Florence Nakalega baada ya kufunga ndoa juzi
Harusi ya mshambuliaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi imeacha historia nchini Uganda akitumia dola 80,000 ( Sh 160,000 Mil ) kwa ajiri ya kuifanikisha iliyofanyika Jumamosi jijini Kampala.
Kiasi hicho kinatosha kabisa kukamilisha usajili wa timu zisizopungua tatu za Ligi Kuu Bara, lakini yeye alitumia fedha hizo kwa ajili ya sherehe, huku Gazeti hili lilikuwa Uganda na kushuhudia kila kitu kilivyokuwa kinaendelea wakati Okwi akimuoa Florence Nakalega.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hamis Kiiza na Nabisubi Julian ndiyo walikuwa wasimamizi wao wa harusi hiyo, ilifungwa katika kanisa la Miracle Centre Cathedral lililopo Lubaga, Kampala.
Baada ya hapo shughuli ya kupiga picha za ukumbusho kwa maharusi, ilifanyika katika hoteli kubwa ya kifahali ya Munyonyo Lesort Beach na kumaliziwa na sherehe kamili kwenye Ukumbi wa Main Exbition Hall uliopo ndani ya jengo la UMA maeneo ya Lugogo.
Okwi alitumia magari saba yalikuwa maalumu kuwabeba maharusi, kati ya hayo matano ni aina ya Jaguar na mawili Brevis.
Hata hivyo, msafara wa harusi hiyo ulipata matatizo baada ya magari mawili yaliyowabeba wasimamizi akiwemo Hamis Kiiza kupata ajali, lakini hakuna aliyeumia zaidi ya mishtuko ya kawaida.
Maharusi wabadili nguo mara mbili
Hapa ndipo kulikuwa na utamu kamili, maharusi waliingia ukumbini majira ya saa 11 jioni, mwanaume walivaa suti za bluu na mwanamke gauni na shela nyeupe kabla ya kwenda kubalisha na kuvaa suti za kaki kwa wanaume na bibi harusi alivaa gauni lenye rangi ya kijivu.
Okwi alipokelewa na wachezaji wenzake waliokuwa wameshika mipira kwa juu yeye akapita katikati yao huku wakicheza na baada ya hapo walikabidhiwa mpira na makocha Sam Simbwa na Moses Basena.
Katika hali isiyo ya kawaida, Okwi alijikuta akidondosha chozi alipokuwa anazungumzia wasifu wa mkewe, Florence na alilia baada ya kuona chozi la mkewe ambaye ndiye alianza kuelezea wasifu wa mumewe.
Okwi alipoulizwa alisema: “Nililia kutokana na furaha kwani tumepita katika mazingira ya kila namna, magumu na raha.
“Nimefurahi sana kukamilisha shughuli hii na sasa nina mke ambaye tutatengeneza familia moja na atakuwa mshauri wangu,” alisema Okwi.
Post a Comment