WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ASHIRIKI IBADA YA KUSIMIKWA ASKOFU MKUU E.A.G (T).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ataitisha kikao cha viongozi wa dini zote hivi karibuni ili wapange na kuainisha ni mambo gani ambayo wanaweza kutoa ushauri kwa Serikali na kupata njia bora ya kuwahudumia Watanzania.
Alitoa ahadi hiyo jana mchana (Jumapili, Februari 7, 2016) wakati akizungumza na mamia ya waumini walioshiriki ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Pili wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Askofu Dk. Brown Abel Mwakipesile iliyofanyika kwenye kanisa la EAGT la Mlimwa West nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alihudhuria ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli alisema: “Hivi karibuni nitaitisha kikao cha viongozi wa dini zote kitakachojumuisha Maaskofu Wakuu, Masheikh na baadhi ya wachungaji ili tukae na kubaini ni nini kifanyike ili kuisadia Serikali namna nzuri ya kuboresha maisha ya Watanzania.”
Akijibu risala iliyosomwa na Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Leonard Mwizarubi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kufanya mapitio ambayo yatawawezesha Watanzania kupata huduma kwa urahisi.
“Katibu Mkuu pamoja na Baba Askofu Mkuu wamegusia suala la upandaji wa gharama za vifaa vya ujenzi pamoja na suala la makazi bora. Mwezi ujao tunaanza vikao vya Bunge vya kupitia bajeti ya Serikali, tutaliangalia hili kwa kumshirikisha Waziri wa Fedha… tutafanya mapitio katika hili ili mwananchi wa kawaida aweze kumudu maisha,” alisema huku akishangiliwa na waumini hao.
Aliwaomba viongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini wake waendelee kuiombea nchi pamoja na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwani kazi ya kutumbua majipu waliyoianzisha ina mitihani mikubwa.
“Kutokana na maombi yenu kwa viongozi wakuu wa kitaifa nina imani Taifa hili litafika tunakotaka liende. Endeleeni kutuombea kwa sababu kazi ya kutumbua majipu ina mitihani mikubwa. Lakini pia napenda niwahakikishie kuwa Serikali hii itatumbua majipu hayo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Hakuna mtu ambaye ataonewa,”alisisitiza Waziri Mkuu.
Kuhusu mgogoro wa kiwanja cha kanisa hilo kilichopo eneo la Ipagala, Waziri Mkuu aliahidi kulishughulikia suala lao Jumatatu( leo ) asubuhi kabla hajaondoka kurejea Dar es Salaam.
“Kesho ( leo) asubuhi nitamuita Mkurugenzi Mkuu wa CDA na kumtaka anipe taarifa sahihi kuhusu mgogoro huu. Najua suala hili liko mahakamani, lakini naamini Mkurugenzi anaweza kuwa kiungo kizuri kati ya wananchi waliojenga eneo hili pamoja na kanisa ambao mnamiliki kiwanja husika”.
“Kama atapata eneo jingine na kupima viwanja, kisha akawapatia hawa wananchi anaweza kuwa amesaidia kuondoa mgogoro huu. Wananchi walienda mahakamani huku wakijua eneo lenu limewekewa uzio, sasa wanagoma kutoka kwa sababu hawana mahali pa kwenda,” aliongeza.
Mapema, akitoa hotuba yake, Askofu Mkuu Dk. Mwakipesile alisema kanisa litaendelea kuiombea Serikali ya awamu ya tano ili nchi idumu katika amani na utulivu.
Aligusia eneo la kanisa lililopo kiwanja na 34, kitalu ‘E’, Ipagala East, Dodoma, ambalo ujenzi wa shule yake umesimama kutokana na mgogoro baina yao na wananchi waliovamia eneo lao kwa kujenga nyumba za kuishi licha ya kuwa eneo hilo lilikwishawekewa uzio.
“Kama kanisa tumeshindwa kukamilisha ujenzi wa shule kwa sababu wananchi hao walifungua kesi mahakamani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Tunaomba uamuzi wa kesi hii uharakishwe,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema kanisa hilo lina majengo 4,670 nchini kote na viwanja 420 ambavyo ni vya kujenga makanisa na vituo vya kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Mwizarubi alisema katika risala yake kwamba wanaiomba Serikali ifikirie kushusha bei ya vifaa vya ujenzi ili wananchi waweze kuwa na nyumba bora za kuishi.
“Maisha bora maana yake ni kuwa na nyumba bora. Tunaiomba Serikali yako ipunguze bei ya vifaa vya ujenzi ili Watanzania waweze kuwa na makazi bora,” alisema huku akishangiliwa.
Post a Comment