Header Ads

Mnyukano wa Halima Mdee na Dk. Mwakyembe Bungeni Jana Febr 2 Kuhusu Sakata La Mabehewa Mabovu.


Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe na Mbunge wa jimbo la Kawe, Halima Mdee (Chadema), jana waliingia kwenye mvutano mkali huku wakitunishiana misuli ya sheria kuhusu kashfa ya ununuzi wa mabehewa 274 yanayodaiwa kuwa mabovu. Ununuzi huo uliofanywa wakati Dk. Mwakyembe alipokuwa Waziri wa Uchukuzi.

Mdee aliibua tena suala la kashfa ya ununuzi wa mabehewa hayo 274 akisisitiza kuwa ni mabovu, wakati alipopata nafasi ya kuchangia katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2011/- 2015/16 ambapo aligusia ahadi ya serikali ya kukarabati reli ya kati  ambayo alidai haijatekelezwa ipasavyo.

Dk. Mwakyembe alikanusha taarifa ya kuwepo kwa mabehewa mabovu kati ya mabehewa hayo 274 yaliyonunuliwa wakati akiwa Waziri wa Uchukuzi.

 “Leo nikimwambia Halima aniletee mabehewa ambayo hayafanyi kazi atashindwa kunionesha,” alisema  Mwakembe

Waziri huyo alieleza kuwa mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo ulitoa mwanya wa kufanya ukarabati au marekebisho katika bidhaa husika ndani ya muda fulani, kipengele kinachojulikana kama ‘defect liability period’. 

Hivyo, alitumia kipengele hicho kufanyia marekebisho mabehewa hayo ambayo alikiri hayakuwa mazuri yalipowasilishwa.

“Mabehewa yote yanafanya kazi kwa sababu yalipoletwa ni mimi mwenyewe nilisema kuna mabehewa ambayo sio mazuri. Nikaunda uchunguzi, kwa sababu tulikuwa na haki chini ya mkataba (defects liability period), ilikuwa ndani ya mwaka mmoja, wakaja wale walioutuuzia mabehewa wakayatengeneza. Sasa yako wapi hayo mabovu?” alieleza Mwakyembe.

Juzi, Mwakyembe alieleza kuwa yuko tayari kujiuzulu ubunge wake kama itabainika kuwa madai ya kashfa hiyo ni ya kweli.

 Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walitaka ripoti ya uchunguzi wa ununuzi wa mabehewa hayo iwasilishwe bungeni huku wakisisitiza kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria ya ununuzi iliyopelekea ununuzi wa mabehewa mabovu.


No comments