Header Ads

MCHUNGAJI KIONGOZI KANISA LA KKKT JELA KWA WIZI

Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Rauya, Zawadiel Maruchu amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la wizi wa kuaminiwa.

Usharika aliokuwa anahudumu mchungaji huyo upo Mambo katika Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Dayosisi ya Kaskazini.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Himo – Moshi, Shaban Mkude baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Kesi hiyo ya jinai namba 417/2015, ilifunguliwa na mlalamikaji Judith Matemba, akimtuhumu mchungaji Maruchu kwa kujipatia Sh8.3 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Kosa hilo ni kinyume na Kifungu namba 304, Sura ya 16 ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2002, kosa ambalo adhabu ni kifungo cha miaka mitatu. Awali, mwendesha mashtaka, Koplo Patrick Mgiriama alidai mahakamani kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 16, 2011 akimshawishi Judith anunue kiwanja eneo la Njiapanda ya Himo.

Siku hiyo mshtakiwa alimfuata mlalamikaji dukani kwake na kumshawishi kuwa kuna kiwanja kinauzwa karibu na Sekondari ya Muungano kwa Sh8.3 milioni.Hakimu alisema mshtakiwa ndiye aliyewachukua mlalamikaji na mumewe na kwenda kuwaonyesha kiwanja hicho na kwa vile mshtakiwa ni kiongozi wa kiroho alimwamini na kukubali kukinunua. Makubaliano ya mauzo hayo yalifanyika nyumbani kwa mchungaji na baada ya kukabidhiwa fedha hizo, alizifanyia sala fupi na kuahidi kumpelekea muuzaji ambaye alimtaja kuwa ni Boniventura Kilawe.

Hata hivyo, ilibainika baadaye kuwa kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na mtu mwingine aliyekuwa na hati za umiliki na jitihada za mlalamikaji kutaka arudishiwe fedha zake hazikuzaa matunda. Hakimu Mkude alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kuuchambua, alimtia hatiani mshtakiwa huyo kwa kosa hilo na kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela. Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa maelezo kuwa anategemewa na familia, ana matatizo ya kiafya na ni kiongozi wa kiroho.

Baada ya kusikiliza maombi ya mchungaji huyo, hakimu alisema ameyazingatia hivyo anamhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela na atakapomaliza alipe fedha hizo.

Jana, mlalamikaji katika kesi hiyo alisema baada ya kutolewa kwa hukumu, ndugu wa mfungwa huyo walitafuta fedha hizo na tayari amelipwa hivyo yatakayoendelea yeye hayamhusu tena.

No comments