Header Ads

Magufuli: Nimeanza kazi

Ikiwa leo ni siku ya 107 tangu Rais Dk. John Magufuli, aanze kazi ya kuwatumikia Watanzania kwa staili yake ya utumbuaji majipu, amesema kazi ndiyo imeanza na ataongeza kasi ya utendaji na kushughulika na mafisadi  ambao wameneemeka kwa jasho la wananchi maskini.
 
Kauli ya Rais inakuja huku akiwa amegusa taasisi, mashirika na wizara mbalimbali za serikali ambazo kwa namna moja, baadhi ya watumishi wameshiriki katika ubadhirifu wa mabilioni ya fedha na makundi mbalimbali wakimsifu kwa kazi aliyoifanya kwa siku 100 tangu aapishwe Novemba 5, mwaka jana.
 
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana na makundi ya wanahabari, wasanii, Tehama na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao walishiriki kwenye kampeni za urais kwa chama chake mwaka jana, kwa lengo la kuwashukuru, Rais Magufuli alisema majipu ni mengi na mengine yanashindwa kutibiwa kwa dawa za kutuliza maumivu.Alisema Tanzania ni tajiri, lakini baadhi ya watu walifika mahali pa kutamani ufisadi zaidi kuliko kumuogopa Mungu na hakuna aliyejali maisha ya Watanzania kwa wingi wao.
 
“Kila unapogusa ni majipu, ukiangalia hujui uanzie wapi, mengine yameiva, mengine yanakaribia kuiva, mengine tumeyatumbua na hayatibiki hata kwa ‘Antibiotic’ (dawa…hatufanyi hivyo kwa kuwa sisi ni wakatili sana au tuna roho mbaya, lakini tunataka mambo yaende na ni lazima yaende,” alisema.
 
Rais Magufuli ambaye aliyekuwa amefuatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri watatu, alisema anapenda kuwa na Tanzania ya kisasa ambayo viongozi wake wanatambua wajibu wao kwa wanyonge na siyo kujinufaisha na familia zao.
 
“Nataka viongozi na watumishi wa umma ambao ni watatuzi wa matatizo ya wananchi kwa kuchukua hatua stahiki kwa wakati na siyo kujiwazia yeye na familia yake,” alifafanua na kuongeza:
 
“Nitaongeza kasi ya utendaji kazi, wanaolalamika walalamike kwa kuwa Watanzania wamelalamika kwa miaka mingi, sasa ni zamu yao. Ni afadhali watu 1,000 walalamike, lakini Watanzania milioni 50 wafurahie nchi yao. Tukiwaacha wengi hata kwa Mungu tutashindwa kujibu.”
 
Dk. Magufuli alisema kampeni zimekwisha hivyo kila Mtanzania kwa itikadi, imani na eneo lake washikamane bila kujali vyama au tofauti za kisiasa kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania mbele na kuweka masuala binafsi nyuma na kwa kufanya hivyo nchi itafikia uchumi wa kati.
 
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, ametumbua majipu katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kwenye halmashauri mbalimbali.
 
Utumbuaji majipu huo umewezesha serikali kupata mapato ya zaidi ya Sh. trilioni 1.5 ambazo zilipotelea mikononi mwa wajanja wachache.
 
Marufuku vibali vya sukari
Rais Magufuli amepiga marufuku utoaji wa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi ili kulinda na kuimarisha viwanda vya ndani ambavyo viliathiriwa kwa kiasi kikubwa cha bidhaa hiyo.
 
Alisema serikali inahubiri kufufua na kuanzisha viwanda, lakini vilivyopo vina changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa kama ilivyo kwenye viwanda vya sukari ambavyo vinashindwa kuzalisha zaidi, kutoa ajira na kununua sukari ya wakulima wa miwa na kulipa kodi kwa serikali kutokana na soko kujaa sukari ya kutoka nje.
 
“Tuna viwanda vya sukari ambavyo vinanunua miwa kutoka kwa wakulima wadogo, vinazalisha sukari na vinatoa ajira pamoja na kulipa kodi, ila ndani ya serikali kuna watu wanatoa vibali vya kuleta sukari nchini huku sukari ya kutosha ipo. Serikali ni moja, unakuta mtu anatoa vibali, watu hawa wanarudisha serikali nyuma…sasa vibali vya kuagiza sukari marufuku hadi kibali maalum,” aliagiza.
 
Dk. Magufuli alisema mbaya zaidi sukari kutoka nje nyingine imeharibika inapoletwa tarehe husogezwa mbele kuonyesha inafaa kwa matumizi.
 
Alisema Watanzania wote bila kujali itikadi, rangi, kabila na dini, wanatakiwa kuisaidia Tanzania kufikia uchumi wa kati kwa kukuza sekta ya viwanda itakayotoa ajira kwa wingi na kukuza uchumi.
 
Awaasa wanahabari
Aidha, aliwataka waandishi wa habari nchini kutanguliza uzalendo mbele kwa kuandika mambo ya kuelimisha na kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake na kuleta maendeleo kwa wananchi.
  
“Kamwe usitegemee shangazi au mjomba kutoka nje aje kuijenga Tanzania. Waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kujenga au kubomoa nchi ndani ya siku chache au kuifanya iwe kisiwa cha amani kwa kuipamba na kila unapochukua kalamu na karatasi kabla ya kuandika lolote anza na Mungu,” alisema.
 
Alisema viongozi ni wawakilishi wa wananchi tu, kwani leo ni zamu yake, lakini kesho atakuja mwingine na kwamba isifike mahali wakaichafua nchi kwa kuwa wote hawana pa kukimbilia.
 
“Tujifunze kwa Mwalimu Julius Nyerere na waasisi wengine ambao kama wangeamua kuweka maslahi yao mbele, hata uhuru usingepatikana, ila kwa umoja wao wakajenga nchi. Tukiamua kujenga nchi, tutafika mbali,” alisisitiza.
 
TPC, Mtibwa wanena  
Baadhi ya wadau wa sukari nchini wamepongeza hatua ya Rais huku wakiomba kushughulika zaidi na njia za magendo ambazo hutumika kuingiza sukari hiyo ikiwa ni pamoja na kufuata sheria ya kuteketeza shehena zinazokamatwa badala ya kuwapa adhabu ya kulipa na kuendelea kuwapo sokoni.
 
Ofisa Mtendaji Utawala Kiwanda cha Sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro, Jaffary Ally, akizungumza  na Nipashe kwa njia ya simu, alisema kwa miaka mitatu viwanda vya ndani vimekandamizwa na sukari ya magendo ambayo huuzwa kwa bei rahisi na kuwalazimu wazalishaji wa ndani kuuza kwa bei ya chini ya uzalishaji. 
 
Alisema sukari hiyo iliathiri mtiririko wa fedha, bei ya miwa inayonunuliwa kutoka kwa wakulima wa nje wa viwanda vya Kilombero na Mtibwa, uwezo wa viwanda kulipa mikopo ya benki, wasambazaji, kuongeza mishahara na marupurupu ya wafanyakazi.
 
Alisema uamuzi wa Rais utalinda na kuimarisha viwanda vya ndani na walaji kwa kuwa sukari ya nje iliingia bila kupimwa na hivyo kuathiri watumiaji pamoja na viwanda kuongeza uwekezaji na upanuzi wa mashamba ya miwa kwa lengo la kukuza zaidi uzalishaji wa sukari nchini.
 
Ally alitoa takwimu za sukari ya magendo iliyoingizwa nchini kuwa mwaka 2012 tani 200,000, mwaka 2013 tani 150,000 na tani 50,000 zililipiwa kodi ya asilimia 10, wakati nchi za Thailand kodi ya sukari ya nje ni asilimia 60 na India ni asilimia 65.
 
Alisema kwa sukari ya magendo kuingizwa nchini kila mwaka, serikali inapoteza kodi ya Dola milioni 40 (sawa na Sh. bilioni 87) na fedha ambazo zingeokolewa zingeingia kwenye maendeleo ya taifa.
 
Kwa upande wa Kaimu Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa mkoani Morogoro, Hamad Yahaya, alisema pamoja na hatua njema ya Rais, lakini ni lazima alinde mipaka ambayo ina njia za panya nyingi zinazotumika kuingiza sukari hiyo.
 
“Tangu Januari, mwaka huu, hakuna kibali cha kuingiza sukari kilichotolewa, lakini soko limejaa sukari ya nje ambayo imeingizwa kwa magendo, hivyo upungufu hauwezi kuonekana, lakini serikali ikibana mianya ya njia za panya, tutafanikiwa kupanua viwanda vyetu, kuongeza ajira na kununua miwa kwa wingi kutoka kwa wakulima kwa kuwa tutakuwa na nguvu ya soko,” alisema.
 
Yahaya alisema licha ya sheria kutamka kuwa mtu anapokutwa na sukari ya magendo afilisiwe, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mwaka jana iliruhusu wahusika kulipa ushuru na kuendelea kuuza sukari hiyo.
 
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, mara kwa mara amenukuliwa akisema kuwa matatizo yaliyopo kwenye sekta ya sukari nchini ni makubwa na yanahitaji kutatuliwa kwa haraka vinginevyo viwanda vilivyopo vitashindwa kuendelea na uzalishaji.
 
Mwaka 2004, viwanda vya Kagera, Mtibwa na Kilombero vilipunguza wafanyakazi 8,000 kutokana na kukosa soko la sukari wanayozalisha.

No comments