JK: Mamluki CCM washughulikiwe.
MAMLUKI waliobaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), siku zao zinahesabika, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, kumuagiza Makamu Mwenyekiti, Tanzania Bara, Philip Mangula kuanza kuwashughulikia.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya 39 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika jana katika Uwanja wa Namfua, mkoani Singida, Kikwete alisema chama hicho kimevuka salama katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba mwaka jana, pamoja na baadhi ya wenzao kuondoka.
“Tunashukuru uchaguzi ulipita na Chama kimevuka salama katika mchakato mzito kinyume na watu walivyotutabiria kifo... haukuwa rahisi kwetu kwa sababu ulizidiwa na kelele na vitisho pamoja na kuwepo wenzetu waliotuhama na kudhani tutakufa lakini hatukutetereka. “Tunajua wako wengine waliobaki kama mamluki, lakini wajue siku zao zinahesabika maana hatutakubali kuendelea kunyonywa damu, natumaini Mangula umeanza kuwashughulikia hawa mamluki,” alisema Mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake.
Uteuzi wa mgombea
Akizungumzia mchakato mzima wa kumpata mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi uliopita, Kikwete alisema alishangaa kuona kwenye vikao vya uteuzi wa ugombea nafasi hiyo, wasaliti wakijipanga kwenye safu ya mbele.
Alisema busara ilitumika katika kikao hicho kwani wasaliti walikuwa wamejipanga kukitikisa chama, lakini ndani ya chama mtu sio maarufu bali chama na maamuzi thabiti ya kumpata mgombea wa nafasi hiyo, ndiyo yaliyokipa chama ushindi.
“Kama tusingekuwa na mgombea hodari na mwenye sifa tusingeshinda, sikuwa na mashaka na uteuzi wa Magufuli na nililisema hilo kwa wanachama sina mashaka naye na hata kwa wagombea wengine tuliowateua,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Alisema wale wote wanaodhani wana umaarufu ndani ya chama, waondoe dhana hiyo kwani CCM siku zote kaulimbiu yake ni chama kwanza mtu baadaye na hata kama mtu ana umaarufu wake na fedha kiasi gani, lazima awe mdogo kuliko chama.
Mafunzo
Akizungumzia mafunzo waliyopata wakati wa uchaguzi huo, Kikwete alisema ni umuhimu wa dhana ya chama kwanza mtu baadaye, kwamba chama hicho mara zote kinapaswa kuwa kikubwa kuliko mtu yeyote, hata awe na fedha kiasi gani.
Amesema katika uchaguzi huo, wamejifunza kwamba umoja wa wanachama wazalendo ndio siri ya ushindi wao kwani hata wasaliti walipotaka kukihujumu chama, umoja wao ulisimama na kushinda.
“Siri ya ushindi wetu ni umoja wetu, watu walivunja makundi baada ya kumtangaza mgombea wetu na kujiunga pamoja ingawa wasaliti waliendelea kuwepo ila hawakufanikiwa, kwa kuwa umoja ulikuwa imara zaidi yao,” alisema Kikwete.
Alitambua makundi yaliyopigania chama hicho, wakiwemo wasanii ambao walizunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi wapigie kura chama hicho na kusisitiza, lazima chama hicho kiendelee kuwajali, kuwaenzi na kuwasaidia katika changamoto wanazokabaliana nazo, hasa mapato yasiyostahili ya kazi zao.
Funzo lingine walilopata, alisema ni utayari wa chama hicho kumtoa mgombea urais mwanamke, kwa kuwa walioshinda katika nafasi tatu bora za kumpata mgombea urais, walikuwepo wanawake wawili, jambo ambalo halijawahi kutokea.
Mbali na kuwa na wagombea wawili wanawake katika nafasi tatu bora za kumpata mgombea urais, Kikwete alisema hata baada ya hapo alipatikana mgombea mwenza mwanamke, ambayo sasa ndiyo Makamu wa Rais, anayemsaidia Rais Magufuli kuendesha nchi.
Kikwete alisema haitashangaza Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akija kuteuliwa kugombea urais, kwa kuwa atakuwa ameshafanya kazi za kumsaidia Rais Magufuli.
Mawazo mbadala
Mbali na mafunzo hayo, Kikwete aliasa chama hicho kwamba lazima kiendelee kuruhusu watu kutoa mawazo na kuvumilia tofauti za mawazo na hiyo ndiyo siri ya uhai wa chama hicho, ambayo ikiondolewa chama kitapoteza uhai wake.
Katika hilo, aliwataka wana CCM kusikiliza maoni ya wananchi na hata maoni ya wasiopenda chama hicho, kwani wanaweza kuwa na jambo la maana la kusaidia Taifa.
Uchaguzi ndani ya CCM
Katika kuonesha kudhamiria kwa CCM kuwashughulikia wasaliti, Kikwete alisema kwa kuwa chama hicho kinafanya uchaguzi wa ndani mwakani, ni vyema wanachama wakatumia fursa hiyo kuwaondoa wasaliti watakaokuwa wamebakia.
Pia amewataka wanachama katika uchaguzi huo, kusafisha chama na kuchagua viongozi wazuri na kusisitiza wale waliochoka wakubali kukaa pembeni, waingie wengine.
Amewataka wanachama hao kuwaondoa wanachama na viongozi wenye mawazo hasi, walioko ndani ya chama kwa lengo la kutafuta vyeo na wanapokosa hukihama chama.
“Tusikubali chama chetu kiwe na watu wenye mawazo hasi na wale wasaka vyeo kuendelea kubaki ndani ya chama, tutumie uchaguzi ujao kusaficha na kukiimarisha chama, tuwanyanyapae wale wenye nongwa, ambao wakikosa cheo wanakihujumu chama,” alisema mwenyekiti huyo.
Kujitegemea
Mbali na uchaguzi wa ndani ya chama hicho, Kikwete pia alitaka chama hicho kuondoka katika kutegemea mapato ya ruzuku na misaada ya wafanyabiashara, kwa kuhakikisha kinakuwa na mapato yake endelevu.
Katika jitihada hizo, alisema wako wanachama wanaokwamisha chama hicho kila mara kinapofanya jitihada ya kuorodhesha mali zake, ambazo zinapaswa kukiingizia mapato hayo endelevu na wanachama hao ni wale wanaotumia vibaya mali hizo kwa maslahi binafsi na waliojimilikisha mali hizo isivyo halali.
Aliwaonya wanachama na viongozi ambao wamejibinafsishia mali za chama, kuacha tabia hiyo kwa sababu ni moja ya njia za kudhulumu chama hicho na wananchama hawatakubali.
Uchaguzi ujao
Mwenyekiti huyo pia alizungumzia umuhimu wa chama hicho kuanza maandalizi ya uchaguzi ujao sasa, kwa wanachama na viongozi kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa wananchi.
Katika ufuatiliaji huo, aliwataka wanachama na viongozi kutoa majibu ya maswali watakayoulizwa, wakikumbuka kuwa kitakachorudi kuomba kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, ni CCM na wala si Serikali.
Alisisitiza Serikali iliyoko madarakani, kuwajali wananchi wote kwani ndio waliowapa ushindi maana wanachama cha CCM pekee wasingetosha kukipa chama hicho ushindi.
“CCM ina wanachama milioni sita na kura alizopata Rais Magufuli ni zaidi ya milioni tisa, sasa utaona kuna kura zaidi ya milioni tatu za wasio wanachama wa CCM, ni vyema Serikali yetu ikawajali wote,“ alisema Kikwete.
CREDIT:HABARI LEO
Post a Comment