Header Ads

Mwakalinga atupwa miaka 30 jela kwa kubaka mwanafunzi.


MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu Newton Mwakalinga, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye umri wa miaka 16 na kumpa ujauzito.
Mshtakiwa huyo pia ameamriwa kupigwa viboko 12, ambapo atapigwa viboko sita akiingia na viboko sita akitoka, pamoja na kumlipa fidia mlalamikaji shilingi milioni moja. Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu John Msafiri, aliyesema kuwa wakati wa usikilizaji wa shauri hilo upande wa Jamhuri ulipeleka mashahidi sita, akiwemo daktari na kwamba baada ya kupitia ushahidi, upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha mashitaka dhidi yake pasi kuacha shaka yoyote na amemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Neema Moshi, aliiomba Mahakama adhabu kali itolewe kwa mshtakiwa kama sheria inavyotaka. Naye mshtakiwa aliomba Mahakama impunguzie adhabu na imfunge kifungo cha nje, kwani hajafanya kosa hilo.
Hakimu Msafiri alisema, “Nakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela, viboko 12 na umlipe mlalamikaji fidia ya shilingi milioni mbili ambapo adhabu hiyo inakwenda kwa pamoja.” Kwa mujibu ya hati ya mashitaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 10, mwaka juzi eneo la Tumbini Chanika wilayani Ilala.
Ilidaiwa mshtakiwa alimbaka msichana mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa), ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha nne na baada ya kupimwa alikutwa na ujauzito.

No comments