January Makamba Atetea Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar.......Asema Watakaoleta Vurugu Damu Za Wazanzibar Zitawalilia.
Serikali imesema uamuzi wa kurudia uchaguzi wa urais Zanzibar ni halali na wa kisheria na kwamba wanaotafuta suluhu nje ya Katiba, wanakosea.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba alipokuwa akihitimisha majadiliano ya kuchangia hotuba ya Rais John Magufuli.
Alisema uchaguzi ulifutwa kisheria na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa Tangazo la Serikali Namba 6587. Makamba alisema Katiba ya Zanzibar, imeeleza wazi kuwa hakuna mamlaka ambayo itahoji uamuzi wa tume, hata kama ni Mahakama. Alisema akidi ilitimia wakati tume inafikia hatua hiyo.
Waziri huyo alisema wanaotaka kutumia suala hilo kuleta vurugu Zanzibar, damu za Watanzania zitawalilia. Alisema viongozi wakuu wa nchi, wamefanya kazi kubwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo na hivyo ieleweke kuwa ZEC na NEC ni tume zinazojitegemea.
Alisisitiza NEC haiwezi kuingilia uamuzi wa ZEC, kwani uchaguzi wa rais uliofanyika kwa siku moja Tanzania Bara na Zanzibar, umekuwa ukiendeshwa na Tume mbili tofauti. Alisema uchaguzi huo, ulifanywa na tume tofauti na hata wino uliotumika katika chaguzi hizo ni tofauti .
Alisema wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuhakikisha kuwa amani na utulivu, vinalindwa Zanzibar katika marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.
Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”.
Post a Comment