Header Ads

Chanzo mauaji ya mapanga mkoani Geita hiki hapa



Simulizi iliyotanguliwa na kunusurika kuuawa. Vipo visa vingi vyenye sababu mbalimbali katika mauaji yanayofanyika kutumia mapanga mkoani Geita.

Wengi wameuawa, kujeruhiwa hata kubaki na ulemavu baada ya kushambuliwa kwa mapanga mkoani humo.

Mmoja wa waathirika wa matukio hayo ni Mwajuma Charles (65) anayesema macho yake ndiyo yalimponza.

“Walinikata mapanga ili waniue, kilichoniponza ni macho yangu mekundu,” anasema mama huyo.

Si Mwajuma peke yake aliyekumbwa na mkasa huo, Salome Mwanzalima (47) mkazi wa  Bungwe,  Kata ya Bulela, pia alifikwa na masaibu hayo, mbaya zaidi yakitekelezwa na jamaa zake.

“Nilikatwa mapanga na ndugu wa ukoo wakitaka waniue ili wachukue mashamba ya urithi,” anasema Salome ambaye wazazi wake walifariki dunia miaka mitano iliyopita, yeye akiwa mtoto pekee.

Kwa mujibu wa Salome, ndugu wa zake hawakufurahi kuona akimilikishwa peke yake mashamba ya urithi yenye ekari 50. Walimuonea ‘donge’ na kutafuta mbinu za kumuua, lakini hawakufanikiwa baada ya kuokolewa na wasamaria wema.

Lakini Mwajuma anasema katika kijiji alichoishi kulitokea kifo cha mtoto wa miaka mitano aliyeliwa na fisi.

Anasema wanakijiji walihusisha tukio hilo na imani za kishirikina, huku wakimtuhumu yeye kuhusika kishirikina katika kifo hicho. Walimuhisi ni mchawi kwa sababu macho yake ni mekundu.

“Wakati wakimfukuza fisi aliyemuua mtoto huyo, walidai alipotea katika mazingira ya kutatanisha alipofika maeneo ya nyumbani kwangu, hiyo ikawa balaa iliyosababisha nishambuliwe kwa mapanga,” anasema Mwajuma.

Katika mkoa huo kuna watu zaidi ya 200 waliouawa na kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga kati ya mwaka 2014-2015.

Ukiwa mkoani Geita, kila siku ukifungulia redio, si ajabu kusikia watu kenda wameuawa kwa kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana katika kijiji fulani.

Pengine taarifa hizo zimekuwa zikikutisha hata kujiuliza; hivi watu wa Geita wana nini, mbona wanauana?

Geita kuna nini?
Ni hivi karibuni, mji wa Geita ulizizima baada ya kutokea mauaji ya kikatili yaliyoacha simanzi kwa familia na wafuasi wa Chadema baada ya mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa, Alphonce Mawazo kuuawa kwa mapanga.

Tuki hilo liliongeza hofu mara dufu kwani Mawazo alichinjwa hadharani, tena mchana kweupe, hali iliyokumbusha wakazi wa Geita matukio mengi ya mauaji au watu kushambuliwa, huku wakibaki na swali “kesho itakuwa zamu ya nani”.

Wakati bado maomboleo ya kifo cha Mawazo yakiendelea, watu wengine wanne wa kaya moja katika Kijiji cha Bugalama mkoani humo, walikatwakatwa kwa mapanga na watu wasiyojulikana kwa imani za kishirikina.

Kwa nini mauaji ya mapanga?
Ajuza Cecilia Kizimba(99), maarufu kwa jina la Bibi Goe, mkazi wa Kijiji cha Nhwiga wilayani Nyang’hwale anasema wakazi wa mkoa huo hawapendi kuona mtu akipata maendeleo.

Mjukuu huyo wa aliyekuwa Chifu wa Wasukuma wakati huo, Chasama Kizimba, anasema kwa asili watu wa kabila hilo wana wivu, uchu wa madaraka, hawapendi kuona jambo baya au mtu akifanikiwa kwa jambo lolote kinyume na mfumo waliojiwekea na kwamba ikiwa hivyo huenda wakamuua mtu huyo.

“Wakati nikiwa mdogo, nilishuhudia watu wengi wakiuawa na wazee wetu waliokuwa watawala, hata wananchi wenyewe. Walikuwa wakiwauwa watu wanaoonekana kuwa na uwezo wa jambo lolote kijijini,” anasema Cecilia.

Anasema, pia, waliwauwa watu waliokuwa wakifika kijijini hapo wakiwa na fikra za kimaendeleo na kuleta mageuzi na hawakutaka mtu mmoja kijijini aonekane kuwa na sauti kuliko wakuu wake.

Cecilia anasema, wakati huo kulikuwa na kundi maalumu kama Dagashida, lililojulikana kama wazee wa kimila, au washauri wa chifu na kazi yao ilikuwa ni kuwaadhibu watu wanaonekana kuwa na kihelehele au washirikina.

Anaeleza kazi ya wazee ilikuwa ni kutoa uamuzi wa mwisho na chochote kilichoamriwa, kilitekelezwa kwa kuwatumia vijana wenye nguvu, waliokuwa wakitambikiwa kabla ya kwenda kuua.

“Wazee hawa (Dagashida), bado wanaendelea na wanatumika mpaka sasa kuua watu wanaonekana au kudhaniwa ni tishio kijijini,” anasema Cecilia.

Anasema wanakijiji wakiona kuna mtu ambaye wanahisi ni mchawi, huwatumia wazee hao, ambao nao hutoa baraka kwa vijana wa kijijini wanaojulikana kwa kazi hiyo, kwenda kuua.

Zakhayo Muyendi (78), mkazi wa mjini Geita, anasema sababu za mauaji hayo kushamiri ni jamii kukosa utu na hofu ya Mungu.

“Matukio yanayoendelea yanatisha, kadri siku zinavyoendelea ndivyo mauaji yanaongezeka. Ninashangaa, watu hapa Geita wamekuwa na roho mbaya kiasi hicho,” anasema.

Muyendi anasema alipokuwa mdogo mauaji hayo yalikuwepo, lakini kwa namna nyingine siyo kama ilivyo sasa.

Mkazi wa Kijiji cha Bulela, Boniphace Flano anasema elimu ndogo ya watu wa jamii ya kisukuma inayofanya waamini masuala ya kishirikina, ndiyo inasababisha mauaji hayo.

“Tangu zamani, sisi Wasukuma, kwetu ni tatizo kusomesha watoto. Wengi hawakwenda shule na suala la kusoma ni mtihani mzito,” anasema.

Flano anasema tangu zamani, wasukuma walijengewa tabia ya kutopenda shule na watu walioonekana kwenda shule waliuawa kwa imani hizo, hivyo watu waliogopa kusoma.

Kamati ya ulinzi na usalama
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya, anabainisha sababu za kushamiri kwa mauaji hayo kuwa ni wivu wa mapenzi na ushirikina.

“Wivu wa mapenzi upo wa aina mbili; kwanza unawahusisha watu wazima, pili unahusisha vijana,” anasema.

Anaeleza kuwa wivu unatokea pale baba ambaye mke wake amezeeka anapoamua kuoa mwanamke mwingine. “Ikishatokea hivyo, huyu mwanamke aliyezeeka hushirikiana na watoto wake kwenda kumuua baba au mke wa baba yao,” anasema Mangochie.

“Wivu huu, unaenda sanjari na imani ya wanawake wengi wa Kisukuma kwamba kuzaa watoto wengi wa kiume ni ulinzi kwao, hivyo mama anapokuwa na watoto wa kiume hushirikiana kumtenga mume, hapo kwenye familia baba anakuwa mpweke,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo baba huamua kuoa mke mwingine.

“Akioa mke mwingine basi watoto pamoja na mama hupanga njama za kumuua ili warithi mali zake,” anasema Mangochie.

Anasema aina ya pili ya wivu inawahusisha vijana wadogo walio katika uhusiano wa ndoa au ya nje ya ndoa na mwanaume au mwanamke anapomfumania mwenzi wake akiwa na uhusiano na mtu mwingine.

“Mara nyingi tukio la kuua kwa mapanga halifanywi na wahusika bali watu maalumu kijijini, ambao kazi yao ni kuua kwa mapanga. Hukodiwa kwa kulipwa kati ya Sh200, 000 au zaidi, wakati mwingine hulipwa ngombe,” anasema Mangochie.

“Ukitokea msako wa kuwakamata, wananchi hawatoi ushirikiano licha ya kuwafahamu na wanaishi nao kijijini,” anasema Mangochie.

Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwassa anasema mauaji hayo hutokea kwa sababu ya imani za kishirikina, zinazotokana na watu kukosa elimu.

“Wananchi wengi huku wanaamini katika ushirikina. Hii inatokana na sababu mbili kuu; ukosefu wa elimu ya kidunia na elimu ya kiroho,” anasema Mwassa.

Viongozi wa dini
Askofu wa Kanisa la African Inland Church(AIC), Dayosisi ya Geita, Mussa Magwesela anasema mauaji hayo hutokea kwa sababu ya nguvu ya ibilisi.

“Ibilisi ameshika roho za watu, amepandikiza chuki, uongo, hasira na roho za mauaji. Wakazi wengi wa Geita hawana Mungu ndani yao,” anasema.

Anatoa wito kwa Serikali kuwalinda raia wake wasio na hatia akiitaka jamii kuwafichua wauaji na mahakama kusimamia haki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Lotson Mponjoli anathibitisha kuwepo kwa matukio hayo akieleza wanajitahidi kukabiliana nayo.

No comments