Header Ads

UJERUMANI YAMSIFU RAIS MAGUFULI KWA KUPAMBANA NA RUSHWA KWA VITENDO.


Serikali ya Ujerumani imeeleza kufurahishwa na kasi ya kupambana na rushwa na ufisadi ya Rais John Magufuli na kuahidi kumpa ushirikiano katika masuala ya maendeleo.

Ujerumani inakuwa nchi ya kwanza ya kigeni kuvutiwa na kasi ya Rais Magufuli ambaye ameonekana kuelekeza nguvu katika si tu kupambana na maovu hayo tangu aapishwe Novemba 5, bali pia kuchochea maendeleo ya watu wenye kipato cha chini.

Aidha, Ujerumani imesema inasubiri kuona vipaumbele vya maendeleo vitakavyoainishwa na serikali ya Rais Magufuli ili iweze kuisaidia utekelezaji.

Pongezi hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Georg Schmidt.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara yake ya siku tano hapa nchini, Schmidt alisema katika kipindi cha mwezi mmoja tu, Dk. Magufuli ameweza kushughulikia masuala muhimu ya kijamii ikiwamo kuboresha huduma za afya na kuwashughulikia wakwepa kodi.

Kasi ya Rais Magufuli, alisema, itasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zitakapokusanywa zitachangia miradi mbalimbali ya maendeleo kama alivyofanya tayari kwenye afya na elimu.

Mkurugenzi huyo alisema ziara yake nchini ilikuwa na lengo la kuangalia hali ya maendeleo nchini baada ya uchaguzi, miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali yake pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi mbili hizo.

Alisema ameshakutana na baadhi ya watendaji wa serikali, wabunge, wanaharakati, watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuitembelea Mahakama ya Haki za Binadamu iliyopo mjini Arusha.

Alisema pia amekuja kuangalia fursa za kibiashara nchini kwa sababu wawekezaji wengi duniani huvutiwa kwenda kuwekeza kwenye mataifa mbalimbali iwapo nchi hiyo ina usalama wa kutosha.

Akizungumzia suala la Zanzibar, Schmidt aliwataka wananchi kuwa na subira wakati mazungumzo yakiendelea katika jitihada za kutatua mgogoro huo.

“Mazungumzo yanaendelea ya usuluhishi tunasisitiza utulivu, amani na tuna imani mwafaka mzuri utafikiwa,” alisema.
Alisema kwa sasa serikali ya Ujerumani itazielekeza fedha nyingi kwa serikali ya Tanzania ili kushughulikia wakimbizi kutoka Burundi wanaokimbia machafuko.

“Tuna jukumu na wajibu wa kushughulikia mgogoro wa Burundi na fedha zilizokuwa zinakwenda Burundi sasa zitaelekezwa Tanzania kwa kuwa wanapokea wakimbizi wengi zaidi,” alisema Schmidt.

No comments