Header Ads

UFAULU DARASA LA 7 WAPANDA.

WAKATI ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba ukipanda kwa mkoa wa Dar es Salaam, imeelezwa kuwa wanafunzi 49,063 sawa na asilimia 83.17 ya waliofaulu mtihani wa darasa la saba mkoani humo wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda wakati akitangaza majina ya wanafunzi watakaojiunga na sekondari mwakani. Mapunda alisema idadi ya waliofanya mtihani ilikuwa 58,989 sawa na asilimia 98.95.
Kati yao, 715 sawa na asilimia 1.20 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali. Alisema kati ya waliofanya mtihani wavulana ni 23,458 na wasichana 25,605 na kwamba ufaulu umepanda kulinganisha na mwaka jana hivyo kuufanya mkoa huo kung’ara na kushika nafasi ya pili ya ufaulu wa juu kitaifa.
“Jumla ya wanafunzi 11,235, wamechaguliwa katika Manispaa ya Ilala sawa na asilimia 72 ya waliofaulu, wakati Kinondoni ni 15,185, sawa na asilimia 83, huku Temeke wanafunzi 10,394 sawa na asilimia 69 ya wanafunzi waliofaulu, “ alisema Mapunda.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DC), Raymond Mushi, aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kusimamia mazingira, maboresho na mfumo mzima wa shule za sekondari yawezeshe wanafunzi waliochaguliwa kusoma katika mazingira mazuri.
CREDIT:HABARI LEO

No comments