Header Ads

Polisi Wauana Kwa Risasi Jijini Mwanza Wakiwa Lindoni.



ASKARI Polisi wa Kituo cha Polisi Nyamagana jijini Mwanza, Konstebo Daud Masunga Elisha, amemuua askari mwenzake, Konstebo Petro Saimon Matiko kwa risasi na baadaye kujiua kwa risasi na kufa papo hapo.

Tukio hilo lilitokea jana saa 8.30 mchana jijini Mwanza katika eneo la Benki ya Posta Tawi la Pamba wilayani Nyamagana huku chanzo cha mauaji hayo kikiwa hakijulikani.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema kitendo hicho si cha kawaida ndani ya jeshi hilo, na kufafanua jinsi mazingira ya tukio lilivyotokea na kusababisha taharuki kwa wananchi na wateja waliokuwa ndani na nje ya benki hiyo.

“Ni kweli kuna askari wawili wamefariki eneo la Benki ya Posta. Katika eneo la benki hiyo kulikuwa na askari wawili waliokuwa lindoni ambao ni PC Elisha na PC Remigius Alphonce mwenye namba H 4291, wakiwa wanaendelea na lindo alifika askari mwingine aliyekuwa amevaa kiraia PC Matiko na kuwasalimia kisha kuingia ndani ya benki kuchukua fedha,” alieleza Kamanda Kamugisha na kuongeza:

“Baada ya dakika tano, Matiko alitoka nje na kuwaeleza askari wenzake kwamba mtandao unasumbua, wakati akieleza hivyo, ghafla askari PC Elisha aliweka chemba risasi ambapo mwenzake PC Alphonce alimhoji mbona unaweka risasi katika hali ya utayari wa kutumika na alijibiwa kwa ufupi kwamba ‘achana na mimi.’

“Ghafla alimfyatulia risasi PC Matiko na kumpiga eneo la bega la kushoto na kutokeza mgongoni na kuanguka chini, kitendo hicho kilimfanya PC Alphonce kukimbilia Benki ya Barclays ili kuomba msaada kwa askari wenzake waliokuwapo lindoni hapo.

“Kabla ya askari hao kufika, ilisikika sauti ya mlio wa risasi na baada ya kurudi alimkuta PC Elisha akiwa amejipiga risasi kwenye paji la uso na kutokea nyuma ya kisogo, tayari akiwa amepoteza maisha.”

No comments