Pengo kuongoza misa mkesha wa Krismasi.
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Policapy Kardinali Pengo leo saa tatu usiku anatarajiwa kuongoza misa ya mkesha wa sikukuu ya Kuzaliwa Yesu Kristo.
Wakati Wakristo wakifanya mkesha wa Krismasi kote nchini leo, wenzao Waislamu wote nchini leo wanaadhimisha sikukuu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), ambapo Kitaifa Baraza litafanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam kuanzia saa tisa alasiri na mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Misa ya mkesha wa Krismasi itafanyika katika makanisa yote yaliyopo jimboni humo na kote Tanzania, lakini kwa Jimbo la Dar es Salaam, Askofu Pengo ataongoza misa hiyo katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph.
Ratiba ya ibada hiyo iliyotolewa na Katibu wa Jimbo hilo, Padri Aidan Mubezi ilisema siku ya Krismasi ambayo ni kesho, Askofu Pengo ataadhimisha misa hiyo katika Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay, Dar es Salaam.
Padre Mubezi alisema kuwa misa hiyo itaanza saa 3 asubuhi na kwamba Wakristo wote wanakaribishwa kusali katika misa hiyo. Alisema Askofu Pengo anawatakia Wakristo wote duniani sikukuu njema ya kuzaliwa Kristo na kwamba washerehekee siku hiyo kwa utulivu na amani.
Pamoja na hayo, jimbo hilo kwa kushirikiana na majimbo mengine duniani, wanasherehekee sikukuu hiyo huku wakiadhimisha mwaka wa Huruma ya Mungu uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francis.
Alisema katika sikukuu hiyo Wakristo wote hususan Wakatoliki, wanatakiwa kufanya matendo ya huruma kwa watu wasiojiweza ili kupata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wa Waislamu, baada ya mkesha wa Maulid uliofanyika jana usiku, leo Baraza la Maulid litafanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, huku Mufti wa Tanzania Shehe Abubakar Zuber akiwataka Waislamu kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo.
Mufti Zuberi alisema ujio wa Mtume Muhammad (S.W.A) ni kudumisha amani na hekima ya kumjua Mungu.
CREDIT:HABARI LEO
Post a Comment