Mchimbaji aliyefunikwa kifusi aopolewa
JITIHADA za kuokoa wachimbaji wawili waliofukiwa na kifusi machimbo bubu ya dhahabu, yaliyopo eneo la Mnadani Kata ya Sangambi wilayani Chunya, zimezaa matunda.
Hali hiyo inatokana na mmoja wa watu hao, kuopolewa akiwa amekufa jana. Wachimbaji madini hao walifukiwa na kifusi Desemba 27 mwaka huu majira ya asubuhi.
Ufukuaji kifusi ili kuwaokoa ulianza Disemba 28 asubuhi baada ya kupatikana kwa mashine ya kufukua kifusi. Hata hivyo, gari lenye mashine hiyo, halikuwa na taa, hali iliyosababisha shughuli hiyo kusitishwa ilipofika jioni na giza kuanza kutanda. Shughuli hiyo iliendelea tena juzi.
Akizungumza na na mwandishi wa habari hizi kutoka eneo la tukio, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bosco Mwanginde alisema ufukuaji wa kifusi ulianza kuzaa matunda majira ya saa 8 mchana baada ya wananchi waliokuwepo, kufanikiwa kuopoa mwili wa mmoja wa wachimbaji hao.
Mwanginde alimtaja marehemu ambaye mwili wake uliopolewa kuwa ni Wambura Makulu, mwenyeji wa Musoma mkoani Mara huku aliyehamia maeneo hayo miaka kadhaa iliyopita.
“Tumefanikiwa kuukuta mwili mmoja. Shughuli ya kuondoa takataka ilionekana kuwa ngumu hivyo ikabidi wananchi waliokuwepo eneo hili kusaidiana na mashine. Na hapo ndipo tumeweza kuukuta mwili mmoja,” alisema.
Mwanginde alisema pamoja na kuukuta mwili huo, shughuli ya kufukua kifusi iliendelea kwa lengo la kumtafuta mchimbaji mwingine, ambaye jina lake halijatambulika. Inasemekana mtu huyo ni mkazi wa wilaya ya Mbozi.
CHANZO:HABARI LEO
Post a Comment