Header Ads

MKE AUA MME KWA KUMCHOMA KISU SHINGONI.

Mwanamke wa Kijiji cha Nyamatoke wilayani Serengeti, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kumuua mume wake kutokana na wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Phillip Kalangi alisema jana kuwa, mauaji hayo yalitokea Novemba 23, mwaka huu jioni katika makazi ya watu hao.

Kalangi alimtaja aliyeuawa kuwa ni Mbiti Maduhu (35) ambaye inadaiwa alichomwa kisu shingoni na mkewe na kumsababishia kifo, baada ya kutokea ugomvi chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.

Alisema mtuhumiwa alikamatwa na wananchi walioshuhudia tukio hilo na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kenyana, ambao walifika na kumchukua.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu za usalama alisema mtuhumiwa na mumewe walikuwa wakinywa pombe za kienyeji klabuni, huku wakishutumiana.

“Mume akawa anamtuhumu mke kuwa anatembea na wanaume wengine, mke naye akimtuhumu mumewe kuwa ana wanawake wengine. Walipomaliza walikwenda mahali pengine na mume akaagiza soda, mke akanywa bia,” alisema shuhuda huyo.

Alisema baada ya kumaliza vinywaji vyao waliongozana na inasemekana njiani waliendelea kuzozana na walipofika nyumbani walianza kupigana.

Shuhuda huyo alisema katika ugomvi huo mtuhumiwa alimchoma kisu shingoni mumewe, hali iliyosababisha anguke chini huku akipiga kelele.

“Alianguka chini huku akipiga kelele, mtuhumiwa akawa anamvutia ndani, wapitanjia walishuhudia tukio hilo wakasaidia lakini mtuhumiwa akiwa ameshikilia kisu alichachamaa na kuwatisha,” alisema.

Kamanda Kalangi alisema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.

No comments