Header Ads

TANESCO:UMEME WA UHAKIKA KUANZIA KESHO IJUMAA MGAWO HISTORIA.



SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) kesho linatarajia kuwasha rasmi mitambo inayotumia umeme wa gesi inayotoka Mtwara, huku ikielezwa kuwa tatizo la upatikanaji umeme wa uhakika, sasa litakuwa historia.
Hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa uunganishwaji wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi mitambo ya kuzalisha umeme ya Ubungo I na II jijini Dar es Salaam, hivyo kuifanya mikoa yote inayotumia umeme wa gridi ya taifa kutokuwa tena na hofu ya mgawo.
Mikoa pekee ambayo haimo kwenye gridi ya taifa ni Mtwara, Lindi, Kigoma, Katavi na Ruvuma, ambayo inatumia mitambo yake yenyewe, wakati mkoa wa Kagera unaunganishwa na umeme kutoka nchi jirani ya Uganda kwa makubaliano maalumu na Tanesco.
Akizungumza jana, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin alisema wananchi watapata umeme wa uhakika kuanzia kesho Ijumaa baada ya mitambo yote ya kuzalisha umeme kwa gesi kuanza kufanya kazi.
Alisema, lakini mitambo ya Ubungo II ambayo imechelewa kuwashwa kutokana na kusubiri kibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ili kusafisha chembechembe zilizopo kwenye bomba baada ya kuchomelewa.
Alisema usafishaji wa chembechembe hizo, ulihitaji kibali kutokana na kushindikana kusafishwa kwa upepo wa kawaida hivyo kutumia nguvu ya gesi na kinachofanywa gesi inayosafisha ikimaliza inaenda angani.
Alisema gesi hiyo inapokwenda angani, ikikutana na chombo cha usafiri, inaweza kusababisha madhara makubwa hivyo ni lazima kupata kibali kwa ajili hiyo. “Kutokana na hali hiyo ilibidi kutafuta kibali Mamlaka ya Anga na tumepata leo (jana), hivyo kesho (leo) kuanzia saa sita mchana hadi saa saba mtambo huu utasafishwa kwa gesi kwani ikiwa chembechembe kidogo itabaki inaweza kuharibu mtambo huo wa gharama kubwa,” alisema.
Severin alibainisha kuwa mtambo huo umetumia injini kama za ndege, ambazo ni rahisi kuharibika kwa kitu kidogo, hivyo umakini unahitajika kuhakikisha hakuna chembe iliyobaki, kwani wanatumia mgandamizo wa gesi wa 30 hadi 35.
Alisema baada ya kukamilika kusafishwa kwa mitambo hiyo yenye mashine tatu, kila moja ikizalisha megawati 33 za umeme, Ijumaa asubuhi itawashwa mashine moja baada ya nyingine na kufanya umeme kuwa wa uhakika.
Msimamizi wa mitambo hiyo, Stanslaus Simbila alisema mashine hizo tatu, zenye kuzalisha megawati za umeme megawati 109, zitafanya tatizo la umeme kwisha, kwani sasa wana gesi asilia waliyopokea kwa kutumia bomba la gesi kutoka Mtwara.
Kwa muda wa wiki moja kuanzia Septemba 7 hadi 14 mwaka huu, kulikuwa na upungufu wa umeme katika mikoa iliyopo katika gridi ya taifa, hivyo kufanya wananchi kukosa umeme kwa nyakati tofauti.
Hatua hiyo ilitokana na kuzimwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme katika eneo hilo la Ubungo mara kwa mara kwa ajili ya kuunganisha bomba la gesi asilia kwenye mitambo hiyo.
Wakati akielezea kuzimwa kwa mitambo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema baada ya kumaliza uunganishaji wa bomba hilo la gesi, upatikanaji wa umeme utakuwa wa uhakika.

Mramba alisema mahitaji ya juu ya umeme nchini ni megawati 910, lakini mitambo hiyo umeme utakaozalishwa utakuwa megawati 1,200.HABARI LEO

No comments