Header Ads

Lowassa Atoa Msimamo Sakata la Richmond....Aahidi Kukomesha Unyanyasaji kwa Raia


Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), amesema utawala wa serikali yake hautanyanyasa wananchi wanaodaiwa kuwa sio raia.

Alikuwa akizungumza jana na wakazi wa Jimbo la Nkenge, wilayani Misenyi walio mpakani na nchi ya Uganda.

Aliwataka maafisa wa Idara ya Uhamiaji kuacha kuwanyanyasa wananchi kwa kigezo kwamba sio raia.

“Katika utawala wangu nitakapo chaguliwa kuwa rais, raia hatanyanyaswa, suala la unyanyasaji litakuwa historia,” alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wananchi.

Aidha, aliwaeleza wakazi hao kuhusu kero wanayoipata kwa kuzuiwa kuuza mazao yao nchini Uganda kuwa akiwa rais, itakuwa ruksa kwa wakulima kuuza mazao yao nje. 
  
Alisema anashangaa kuona wananchi wanazuiwa kuuza kahawa yao Uganda ambako bei yake ni nzuri huku wakitakiwa wauze hapa hapa nchini kwa bei nafuu.

“Serikali yangu kwanza itaondoa kodi zote kwa mazao ya wakulima na kuwaruhusu wayauze popote pale wanapotaka ndani na nje ya nchi.
 
“Mkulima anayetaka kuuza mazao yake Uganda, ruksa. Tutaondoa kodi zote kwa wakulima...kwa nini Waganda watushinde,” alihoji.

Alisema serikali yake itatoa kipaumbele kwa sekta ya elimu, kilimo cha kisasa na cha kibiashara na kuzingatia maslahi bora ya walimu na wafanyakazi wengine.

Kuhusu tatizo la maji alisema kama aliweza kuyatoa maji Ziwa Viktoria na kuyapeleka Kahama na Shinyanga hatashindwa kuwapatia maji kutoka Mto Kagera.

“Suala la maji Mto Kagera sio tatizo, nilishughulika na maji toka Ziwa Victoria na kuyapeleka Shinyanga na Kahama, sembuse hapa,”alitamba. 

Azungumzia  Sakata  la  Richmond
Akihutubia  Maelfu  ya wakazi  wa  Bukoba  Mjini jana Katika Uwanja  wa Gymkhana,Lowassa aliwashangaa wanaomhusisha na sakata la Richmond na kusema, “Siwajibu ng’o” na kupeleka jukumu hilo kwa wananchi akiwataka wawajibu kwa kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 25, mwaka huu awe Rais wa Awamu ya Tano.

Aliwataka Watanzania watakapoulizwa jambo lolote kuhusu Richmond wajibu kwa kusema, “acha fitna na uongo namchagua Lowassa”. 
  
Sumaye:  CCM  Wana  Kiburi
Naye Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, alisema CCM ni chama cha ajabu kilichojaa kiburi kwa raia wake.
 
Alisema kiburi cha CCM kinatokana na kujiona kuwa kipo kwa ajili ya kutawala. Alisema tangu wajiondoe CCM na kujiunga na upinzani, wametembea nchi nzima na hakika wameona wananchi wameikataa CCM na wanahitaji mabadiliko.

Alisema CCM ni lazima itoke madarakani na wananchi wanatakiwa kutumia kura zao kuing’oa.

“Wananchi ndio watakaoamua kumpigia Lowassa kura za ndio, sasa hiki kiburi cha CCM kusema hawataachia madaraka kinatoka wapi. 
  
“Wewe ni nani ambaye utasema hatutawaachia nchi wapinzani...wewe ni nani zaidi ya maamuzi ya wapiga kura,” alisema.

 Alisema chama tawala mara zote ndicho kinachozua vurugu kwa kung’ang’ania kubaki madarakani.

No comments