Header Ads

Kauli ya UKAWA Kususia Uchaguzi Yaishtua NEC.


Tume  ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeshtushwa na kauli  iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwamba watasusia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Hata hivyo, Nec imetetea kauli iliyotolewa  na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Mgombea urais  ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, kwamba CCM haitakubali kuiachia Ikulu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema kauli hiyo iliyotolewa na kiongozi wa chama kikubwa iliwashtua na kwamba katika vipindi vyote vya uchaguzi vilivyopita, hawajawahi kukumbana nayo.
  
Hata hivyo, Jaji Lubuva alisema baada Nec kufuatilia, ilibaini  kuwa kilichosemwa na Bulembo, hakiendani na kauli  iliyotolewa na Mbowe. 

Jaji Lubuva alisema kauli iliyotolewa na Mbowe si tu kwamba inashtua, lakini  ni hatari kutolewa katika kipindi hiki muhimu cha uchaguzi ambacho Watanzania na nchi nyingine,  zinaamini kwamba uchaguzi utafanyika katika hali ya amani na utulivu. 
  
Lakini alisema baada ya kufuatilia, wamebaini kuwa kauli iliyotolewa na Bulembo katika mkutano wa kampeni za CCM mjini Kigoma ilikuwa ni ya kisiasa na si vinginevyo.

“Bulembo katika kauli yake hajasema kwamba hata kama Nec ikitangaza matokeo CCM wakiwa wameshindwa,  hawatakuwa tayari kuwaachia Ikulu Chadema. Alikuwa anamaanisha kuwa watawashawishi wapiga kura wao wasiwapigie kura ili wasipate nafasi ya kwenda Ikulu,” alisema. 
  
Alisema  kauli iliyotolewa na Mbowe na Bulembo zinakinzana na kwamba baada ya kufuatilia walizinukuu.

“Kukataa matokeo ya uchaguzi hata kama umeshindwa kihalali ni uhaini,” alisema Jani Lubuva.

“Hii ni kauli ya kisiasa kama ambavyo Chadema nao wamekuwa wakitamka kwamba hii ndiyo awamu ya mwisho kwa CCM kukaa madarakani,” alisema Lubuva.

Kadhalika, Jaji Lubuva alikemea na kulaani kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na wagombea, viongozi  wa vyama vya siasa na makada wake katika kampeni zinazoendelea kote nchini.



No comments