Header Ads

BASATA YAONYA LUGHA CHAFU, MAADILI HUSUSAN KATIKA KIPINDI HIKI CHA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.

KATIKA siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi la wasanii kuvunja maadili, kukaidi adhabu na kutumia lugha chafu kwa makusudi katika kazi za Sanaa hususan muziki hali ambayo imezua malalamiko, masikitiko na hofu kwa jamii ambayo ni walaji wa kazi za Sanaa.
Lugha hiyo chafu ambayo inajidhihirisha kwa matusi ya wazi, maneno ya uchochezi, kashfa, kejeli, dharau na udhalilishaji wa kada mbalimbali za kijamii wakiwemo viongozi wa kitaifa inaonesha wazi kulenga katika kuigawa jamii na kufifisha amani, upendo, uzalendo na ustaarabu tuliokuwa nao watanzania.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa misingi ya Sanaa Duniani kote kazi zote za Sanaa zinapaswa ziwe ni zenye kuonya, kuelimisha, kuadabisha, kukosoa, kuburudisha, kuhamasisha na kuchochea maendeleo chanya katika jamii na siyo kuigawa au kuivuruga jamii.
Ndiyo maana msanii anayefanya kazi zake kwa kuzingatia misingi ya Sanaa anatambuliwa kuwa ni kioo cha jamii, kiongozi na pia ni mwalimu wa yale yote yaliyo mema katika jamii inayomzunguka.
Kinyume na misingi hiyo ya Sanaa, baadhi ya Wasanii, studio za kurekodia na kutengenezea muziki, vyombo vya habari vya kielektroniki na mitandao ya kijamii ama kwa kutumiwa au kwa utashi wao binafsi wamekuwa wakijihusisha na Sanaa zenye viashiria vya uchochezi na kuvunja misingi ya weledi katika Sanaa hususan katika kipindi hiki cha kampeni na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Aidha, baadhi ya Wasanii wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya vyama vya Siasa au wagombea na kujikuta wakitumiwa vibaya na kuvunja misingi ya Sanaa kwa faida za kisiasa. BASATA linapenda kutoa maagizo yafuatayo:
1. Wasanii wana haki zote za kikatiba na kidemokrasia kushiriki shughuli za Siasa lakini wanawajibika kwa kiwango cha hali ya juu kulinda misingi ya weledi, maadili, miiko na hadhi yao kama inavyofanyika katika tasnia zingine.
2. Wasanii wanapaswa kutambua kwamba kuna maisha na Taifa baada ya uchaguzi mkuu. Umoja wa kitaifa na umoja baina ya wasanii wa kada zote za Sanaa ndiyo utakuwa msingi mkuu wa kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla pasipo kugawanyika katika misingi ya itikadi za kisiasa
3. Wasanii wasitumie nafasi na umaarufu wao kuligawa taifa, kukashifu viongozi wa kitaifa, kudharau mamlaka, vyama na makundi mbalimbali katika jamii kwa kile kinachoitwa ushabiki wa kisiasa. Ieleweke kuwa Serikali haitafumbia macho wale wote watakovunja sheria, kanuni na taratibu. Tukumbuke kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.
4. Ijulikane kuwa wasanii kama kundi muhimu katika kipindi cha kampeni za kisiasa ni sawa na watu wengine wanaopewa kazi ili kutimiza lengo lililokusudiwa. Wasanii wasitumiwe kama vyombo tofauti na watu wengine.
BASATA linatoa onyo kali kwa msanii yeyote atakayeendelea kukaidi, kuvunja maadili na kusambaza kwa njia yoyote ile kazi ya Sanaa yenye ukengeufu wa maadili.
BASATA linawatakia wasanii wote utekelezaji mwema wa maagizo haya lakini kubwa kuliko yote kutambua kwamba tunatakiwa kujenga mshikamano, umoja wa kitaifa na kustawisha amani tuliyonayo ambapo ikitoweka itaathiri ufanisi wa Wasanii na kuirejesha itatugharimu sana.
Sanaa itumike kulinda amani, kujenga upendo, umoja wa kitaifa na mshikamano baina ya makundi mbalimbali ya kijamii.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA

No comments