Header Ads

TCRA:TUMEJIDHATITI KUWASHIKISHA ADABU.

MAMLAKA ya Mawasiliano (TCRA) imeendelea kuhadharisha umma dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ikisema imejizatiti kwa kuwa na vifaa madhubuti na wataalamu kukabili wimbi la wanaosambaza ujumbe wa uchochezi katika kipindi kuelekea uchaguzi mkuu.
Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema Serikali haitafumbia macho mameneja na wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano serikalini watakaoshindwa kuzuia wizi wa taarifa.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa kongamano la wataalamu wa mfumo wa kompyuta lenye lengo la kujadili mbinu za jinsi ya kujilinda na uhalifu wa mitandao.
Semina hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Usajili Norway (NRD) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam jana Mtendaji Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba alisema watu wanaosambaza taarifa za uchochezi kupitia intaneti na mitandao ya jamii, waache mara moja kwani hakuna atakayekwepa mkono wa sheria.
Alisema, TCRA imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na vyombo vya usalama ikiwamo Polisi, Kitengo cha Kupambana na Uhalifu wa Mitandao. Aliwataka watumiaji wa mawasiliano kuwa na matumizi mazuri ya teknolojia hiyo.
“Tumejipanga vilivyo kushirikiana na vyombo vyote vya dola kuhakikisha tunawanasa wote watakaohusika. Serikali ina mkono mkubwa, mtu yeyote asifikiri anaweza kusambaza taarifa za uchochezi asikamatwe,” alisema.
Katika hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi Sefue iliyosomwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali (e-Government) Ofisi ya Rais na Utumishi wa Umma, Dk Jabiri Bakari, alisema serikali itawachukulia hatua za kisheria mameneja na wataalamu wa IT ambao watatoa mwanya wa wizi wa taarifa.
Aliwataka kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kulingana na maadili ya taaluma.
“Ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuwa na ufahamu wa madhara ya mifumo hafifu na ufungaji wenye kasoro wa mifumo ya usalama ya mitandao ambayo inaweza kutoa mwanya kwa taarifa muhimu za serikali au taasisi ya umma kuibwa hivyo kuvuruga ufanisi wa taasisi hiyo,” alisema.
Aliongeza: “Tukilindana na kila wizara, idara, wakala na kampuni au shirika katika sekta binafsi, nina imani mkutano huu mtapata ujuzi zaidi ambao mtakwenda kuutumia katika taasisi zenu.”

Naye Mtendaji Mkuu wa NRD, Sebastian Marondo alisema mshikamano wa pamoja kwa serikali, sekta binafsi kama mabenki na kampuni za simu unahitajika ili kufikia malengo ya kukomesha, kujikinga au kukinga biashara zao katika uhalifu wa mitandao.HABARI LEO.

No comments