MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema anasumbuliwa na uchovu na ametakiwa na madaktari kupumzika kwa takribani saa 48 bila usumbufu wowote. Mbowe alisema hayo Dar es Salaam jana wakati alipozungumza na waandishi wa habari Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikopelekwa juzi baada ya kujisikia vibaya kiafya. Alisema katika shamrashamra za mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa, kuchukua fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ghafla hali yake ilibadilika, akahisi kizunguzungu na kukimbizwa Hospitali ya Dk Plaza kabla ya kuhamishiwa MNH. “Madaktari walinipima na kubaini kuwa nasumbuliwa na tatizo la uchovu kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu usiku na mchana na kwa jinsi mwili wa binadamu ulivyo, umeshindwa kuhimili,” alisema Mbowe. Alisema kwa sasa afya yake imeimarika na anaendelea vizuri, ingawa ametakiwa kupumzika kwa siku hizo mbili na baada ya hapo ataendelea na majukumu yake kama kawaida. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dk Tulizo Sanga, alisema Mbowe aliwasili hospitalini hapo jana. Alisema alipokewa na kuhudumiwa na madaktari wapatao wanane, waliompima na kumpatia tiba baada ya kubainika kuwa tatizo ni uchovu.
Post a Comment